Habari

Imewekwa: Apr, 20 2026

Waziri Mkuu Aweka Jiwe la Msingi Mradi wa Miji 28 Chamwino

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa miji 28 wenye thamani ya Shillingi bilioni 17.2, katika mji wa Chamwino, Dodoma.

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za mradi huo wa maji, na kuipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia vizuri utekelezaji.

"Nimpongeze Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa mradi huu kwani maji hayana mmbadala, Niipongeze Wizara ya Maji, mnafanya kazi nzuri sana katika miradi ya maji, tunaambiwa kwenye ripoti na tunaona kwa macho kazi inavyoendelea, tumeenda Ruangwa kule Lindi tumeona, tumeenda Singida tumeona, tumeenda Mpanda tumeenda kila mahali tumeona miradi mikubwa ya fedha nyingi inaendelea vizuri. Nikupongeze Mhe. Aweso, na Katibu Mkuu mnafanya kazi nzuri sana, mmefuta visima hewa, mmefuta miradi hewa" Waziri Mkuu Dkt. Nchemba amesema.

Ametoa agizo kwa wakandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ya maji kuhakikisha wanawalipa stahiki zao wote wanaofanya nao kazi ikiwemo vibarua kwakuwa serikali imeshatekeleza jukumu lake la kutoa fedha kwa Mkandarasi.

Ametoa angalizo kwa wakandarasi wote watakaoshindwa kutekeleza hawatopewa tena mradi hapa nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Wizara ya Maji itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika. “Kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi na tayari vijiji 10,758 vimeshafikiwa na huduma ya maji safi na salama na vimebaki vijiji 1,575.”

Mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji utahudumia wananchi zaidi ya elfu 60 wa Msanga, Buigiri, Mtumba na Chamwino.

Utekelezaji wa mradi umefika asilimia 70.2 na utazalisha lita za maji milion 7.7 kwa siku na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 91 hadi asilimia 100.

Mahitaji ya maji katika eneo hilo ni lita milioni 7.5 kwa siku wakati upatikani wa sasa wa maji kwa siku ni lita milioni 4.8

Kitengo cha Mawasiliano