Habari
Mikutano mikubwa ya wadau wa sekta ya maji kufanyika Dodoma
Wizara ya Maji inawatangazia wadau wa sekta ya maji kuwa Mkutano wa Mwaka wa Tisa (9) wa Bodi za Maji za Mabonde, Mkutano wa Saba (7) wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi wa Rasilimali za Maji, pamoja na Uzinduzi wa Bodi ya Tano (5) ya Taifa ya Maji, utafanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 27 hadi 30 Januari, 2026.
Kaulimbiu ya Mikutano ni “Uhakika wa Maji kwa Maendeleo ya Taifa: Utekelezaji wa Dira 2050 katika Ustahimilivu, Usawa na Uendelevu.” Kauli mbiu hii inalenga kuchochea na kuharakisha uwekezaji katika uhakika wa maji na utekelezaji wa malengo ya usimamizi endelevu wa rasilimali za maji chini ya Dira 2050.
Mikutano hii ni muhimu kwa kuzingatia kuwa rasilimali za maji ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, uendelevu wa mazingira, ustawi jamii pamoja na ukuaji wa uchumi. Kwa kutambua mchango huo, Serikali imekuwa ikitekeleza mageuzi makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 25, yakilenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji, kukuza matumizi endelevu, na kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mageuzi haya yamejikita katika utekelezaji wa Mipango Jumuishi ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji (IWRMD) chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP), unaosisitiza ushirikishwaji wa wadau, matumizi yenye usawa ya rasilimali, na ulinzi wa vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Juhudi hizi zinaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 (DIRA 2050), inayotambua rasilimali za maji kama mhimili wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Dira hii inahimiza matumizi bora ya rasilimali, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na majanga, nishati safi, kukuza kilimo chenye tija, viwanda, pamoja na uchumi wa buluu na kijani, sambamba na ujenzi wa taasisi imara, zenye uwajibikaji na mtazamo wa muda mrefu.
Katika muktadha huo, Mkutano Mkuu wa Tisa wa Mwaka (AGM) wa Bodi za Maji za Mabonde ni jukwaa la kimkakati linalowakutanisha Bodi za Maji za Mabonde, Bodi ya Taifa ya Maji, Wizara ya Maji, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya maji. Lengo kuu la mkutano huu ni kutathmini utendaji wa Bodi za Maji za Mabonde kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, kujadili mafanikio na changamoto, na kuweka mwelekeo wa kimkakati kwa kipindi kijacho.
Mkutano huu pia unalenga kuoanisha mipango ya taasisi za sekta ya maji na ajenda mpya za maendeleo ya taifa, ikiwemo DIRA 2050, Mpango wa Mtazamo wa Muda Mrefu, na Mpango wa Mkakati wa Miaka Mitano unaotarajiwa (2025/26–2029/30), hususan wakati ambapo utekelezaji wa WSDP unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026.
Aidha, Mkutano wa Tisa wa AGM unabeba tukio muhimu la kitaasisi kupitia uzinduzi wa Bodi ya Taifa ya Maji ya Tano, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha misingi ya usimamizi bora, uwazi na uwajibikaji katika sekta ya rasilimali za maji.
Sambamba na hilo, Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka utafanyika, ukilenga kujadili mikakati ya kuimarisha uhakika wa maji nchini, kwa kushirikisha wadau kutoka sekta za maji, mazingira, afya, kilimo, nishati, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na wadau wakuu wa rasilimaliza maji.
Wizara ya Maji inakaribisha wadau wote wa sekta ya maji, vyombo vya habari, washirika wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wadau wengine kushiriki na kufuatilia mkutano huu muhimu, unaoweka msingi wa mustakabali endelevu wa usimamizi wa rasilimali za maji nchini Tanzania.

