Habari
Waziri Mkuu Aitaka Wizara ya Maji Kutatua Changamoto ya Upotevu wa Maji
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameielekeza Wizara ya Maji kuchukua hatua madhubuti ili kupata ufumbuzi wa changamoto ya upotevu wa maji, akisisitiza kuwa hali hiyo inaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Wizara ya Maji wakati wa ziara yake ya kikazi katika Makao Makuu ya Wizara hiyo yaliyopo Dodoma. Amesema kuwa kiwango cha upotevu wa maji kimefikia hatua inayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivyo, ni muhimu Wizara ikaweka mikakati madhubuti ya kudhibiti upotevu wa maji kwa kutumia teknolojia za kisasa, kuboresha usimamizi wa mifumo ya maji, pamoja na kuongeza uwajibikaji kwa mamlaka za maji,” Dkt. Nchemba amesema.
Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya katika kutimiza lengo la Kumtua Mama Ndoo Kichwani. Amewahimiza watumishi wa sekta ya maji kuongeza juhudi na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, akibainisha kuwa Serikali imewawekea mazingira bora ya kazi.
“Nimefurahishwa na mazingira yenu ya kazi, kuanzia jengo, ofisi za watumishi hadi mazingira ya nje. Hii inaonesha namna Serikali inavyowajali watumishi wake ili waweze kufanya kazi katika mazingira rafiki na hivyo kuongeza ufanisi,” Dkt. Nchemba amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa Wizara hiyo, jambo linalochangia kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Aidha, amesisitiza kuwa Wizara ya Maji imejiwekea mikakati madhubuti ya kuipeleka Sekta ya Maji katika hatua nyingine, kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji inawafikia Watanzania wote.

