Habari
WATAALAMU WA RUWASA WAPATIWA MAFUNZO YA UENDESHAJI NA MATENGENEZO SKIMU ZA MAJI
Meneja wa RUWASA mkoa wa Arusha Mha. Joseph Makaidi amefungua mafunzo kwa wataalam wa RUWASA yaliyoanza leo Machi 2, 2026 ambapo amesema kuwa kipimo cha kweli cha mafanikio ya mradi wa maji siyo siku ya uzinduzi, bali ni uwezo wa mradi huo kutoa huduma kwa uendelevu kwa miaka mingi ijayo hivyo mafunzo ya uendeshaji na matengenezo ni muhimu ili kuwa na huduma endelevu ya majisafi vijijini.
Alibainisha kuwa RUWASA kwa sasa inaelekeza nguvu kwenye teknolojia ya kusukuma maji kwa nishati ya jua (Solar-Powered Systems) na utafiti wa maji chini ya ardhi, hivyo mafunzo hayo ya uendeshaji na matengenezo (O&M) ni mkakati muhimu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya kudumu.
Mratibu wa Wadau wa Maendeleo wa RUWASA Dkt. Shauku Kihombo alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano kati ya RUWASA na Shirika la Global Water Center la nchini Marekani ambapo awamu ya kwanza ya mafunzo kwa Mikoa 11 ya Tanzania Bara ni kuanzia tarehe 2 hadi 6 Machi, 2026 huku awamu ya pili ikitarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 9-13 Machi, 2026 ikihusisha wataalamu kutoka mikoa 14 pamoja na RUWASA Makao Makuu.

