News

Posted On: Nov, 19 2026

Tanzania yang'ara COP31, miradi ya hewa ukaa Manyara yazalisha sh. Bilioni 1.62

News Images

Tanzania imepongezwa kimataifa kwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya kupunguza hewa ukaa (Carbon Credit Projects) ambapo Wizara ya Maji mkoani Manyara, mradi umewezesha kupatikana kwa Shilingi bilioni 1.624 kutokana na biashara ya hewa ukaa mwaka wa fedha 2023/24.

Pongezi zimetolewa Novemba 17, 2026, katika mkutano wa pembezoni uliofanyika katika Banda la Italia, wakati wa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) jijini Antalya, Uturuki.

Meneja wa Programu wa Shirika la OIKOS Tanzania, iliyopeperusha bendera ya nchi kimataifa Bi. Lara Beffasti, ameutaja mradi wa Manyara kuwa mfano bora wa utekelezaji wa miradi hiyo ikilinganishwa na maeneo mengine barani Afrika.

Mradi unatekelezwa na asasi ya OIKOS EAST AFRICA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji kupitia Wakala ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) Manyara ukihusisha skimu za maji 65 katika wilaya za Simanjiro, Kiteto, Mbulu, Babati na Hanang’, zinazohudumia zaidi ya wananchi 300,000.

Mapato yaliyopatikana yanatarajiwa kutumika katika uendeshaji, matengenezo na upanuzi wa skimu hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa huduma ya maji safi na salama.

Wizara ya Maji inaongozwa katika mkutano huo na Naibu Katibu Mkuu, Bi. Rose Ambrose, ambapo umepokea pongezi kwa niaba ya Waziri wa Maji.

Mafanikio hayo yamekua chachu kuvuta wadau wa kimataifa wa biashara ya hewa ukaa kwa kuonesha nia ya kuwekeza katika Sekta ya Maji nchini, hususan katika mikoa 24 ambayo bado haijanufaika na programu hiyo.

Hatua hiyo inaendeleza jitihada za Serikali katika kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kwa ili kuboresha huduma ya maji nchini, ikiwemo Hati Fungani ya Kijani (Green Bond), maandalizi ya Hati Fungani ya Miundombinu ya Maji (Water Infrastructure Bond) kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji na sasa biashara ya hewa ukaa (Carbon Credit).