Habari

Imewekwa: Sep, 13 2025

​Tanzania na Kenya waungana kupanda miti kulinda Mto Mara

News Images

Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Thecla Mkuchika amewaongoza wadau wa bonde la Mto Mara kutoka Tanzania na Kenya katika zoezi hilo la upandaji miti rafiki wa maji na kusimika vigingi vya mpaka wa Mto katika Kijiji cha Kirumi Wilayani Butiama Mkoani Mara.

Kazi imefanyika ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mto Mara ambayo kilele chake ni Septemba 15.

Mto Mara unaanzia milima ya Mau nchini Kenya hadi ziwa Victoria nchini Tanzania.

Amesema zoezi la upandaji miti na ulinzi wa mto linapaswa kuwa endelevu kwa kila mwananchi anayekaa katika bonde la Mto Mara kutokana na umuhumu wa mto huo kwa jamii inayouzunguka. Aidha amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Aziza Baruti kuhakikisha anasimamia kuhakikisha miti hiyo inatunzwa. Pia kuhakikisha wakulima na wafugaji wanazingatia sheria inayowataka kufanya kazi zao nje ya eneo la hifadhi ya mto.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Renatus Shinhu amesema miti iliyopandwa kwa siku ya leo ni miti 3,000 huku zoezi likiendela ili kufikisha miti 8000. Amesema Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha Bonde hilo linaendelezwa na kwamba hawatasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote anayeharibu bonde hilo.

Naye Mwakilishi kutoka Kenya, Galfen Omuse amesema Mto Mara umekuwa sehemu ya kuyaunganisha mataifa ya Tanzania na Kenya katika ushirikiano. Ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha nia ya dhati ya kuhakikisha mto mara unatunzwa na kuendelezwa.

Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa kupokezana kati ya Tanzania na Kenya yakilenga kushirikishana njia mbalimbali za kuhakikisha mto Mara unatunzwa na kuendelezwa na faida ya pande mbili za nchi