Habari

Imewekwa: Aug, 06 2019

Serikali Kusaini Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Mugango-Kiabakari

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD) zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mugango-Kiabakari katika mkoa wa Mara.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametoa kauli hiyo akiwa kwenye ziara ya kikazi katika kufuatilia na kukagua miradi ya maji inayotekelezwa mkoani Mara.

Amesema mkataba huo utakaogharimu Dola za Marekani milioni 30.69 unatarajiwa kusainiwa tarehe 15 Agosti, 2019 unalenga kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya Mugango, Kiabakari na Butiama, na kwa sasa hatua ya usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni umekamilika na taratibu za kumpata Mkandarasi zinaendelea.

Kazi ya uboreshaji ya mradi huo mkongwe ulioanza mwaka 1974 itakapokamilika utanufaisha wananchi wapatao 80,000 waliopo katika eneo la mradi pamoja na vijiji 13 vilivyopo ndani ya kilomita 12 kutoka bomba kuu. Serikali imetenga Shilingi bilioni 8.5 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Aweso amesema Mtaalam Mshauri kutoka Kampuni ya WAPCOS Ltd ya India tayari ameanza kazi ya upembuzi yakinifu kwa miradi ya maji katika miji ya Rorya, Tarime na Mugumu mkoani Mara tangu tarehe 1 Juni, 2019 na atakamilisha kazi hiyo ifikapo tarehe 31 Agosti, 2019.

Akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kumaliza tatizo la maji katika maeneo yote yaliyo pembezoni mwa Ziwa Victoria.

Miji ya Rorya, Tarime na Mugumu ni miongoni miji itakayonufaika na Mradi wa Maji wa Miji Mikuu ya Wilaya 29 inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 kupitia Benki ya Exim ya India.

Kitengo cha Mawasiliano

Agosti 6, 2019