Habari
Rais Samia Aandika Historia Sekta ya Maji Simiyu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameandika historia mpya katika Sekta ya Maji nchini kwa kufanya uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Lamadi wenye thamani ya Shilingi bilioni 12.83 na kuweka jiwe la msingi kwa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wenye thamani ya Shilingi bilioni 440, yote mkoani Simiyu.
Katika hafla hiyo ya kihistoria Rais Samia amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo miwili utaboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya majisafi na salama pamoja na usafi wa mazingira kwa wakazi wa miji ya Lamadi na Nyashimo kwa Mradi wa Lamadi, pamoja na Busega, Itilima, Bariadi, Lagangabilili na vijiji 103 kwa awamu ya kwanza ya Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
“Ninaamini kuwa ujenzi wa mradi wa Lamadi niliouzindua, na huu niliouwekea jiwe la msingi hapa Nyashimo kwa pamoja itaboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Mkoa wetu wa Simiyu,” Rais Samia amesema.
Rais Samia ameitaka Wizara ya Maji kuendelea kushirikiana na viongozi wa mikoa ili kufanikisha mpango wa kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.
Aidha, Rais Samia ametoa shukrani kwa wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund - GCF), Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya Ujerumani ya KfW ambao wanashirikiana nasi katika utekelezaji wa mradi huu mkubwa kwa gharama ya Shilingi Billion 440.
Pia, ametoa shukurani kwa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank- EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ambao wamegharamia ujenzi wa mradi wa maji Lamadi kwa gharama ya Shilingi Bilioni 12.83. Akisisitiza ushirikiano wao umekuwa muhimu kufanikisha miradi hiyo ya kimkakati.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameagiza juhudi za kuhifadhi mazingira ziendelee kufanyika kikamilifu kwa kushirikisha sekta zote kwa kuwa uhifadhi wa mazingira ni msingi wa uendelevu wa upatikanaji wa maji, kuwezesha shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo kilimo, viwanda, ufugaji, uvuvi na utalii.
Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kuwa kati ya vijiji 12,318 vilipo nchini vijiji 10,779 vimefikiwa na huduma ya maji na vijiji 1,539 vilivyobaki vinataegemewa kufikiwa baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya kimkakati ikwemo mradi huu wa Simiyu na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa nchini kote.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesisitiza Wizara itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara, mkoa, halmashauri na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira ili kuhakikisha uendelevu wa miradi ya maji nchini.
Mradi wa Maji wa Lamadi ni sehemu ya Satellites Town Projects ambapo awali, mradi huo ulikuwa na lengo la kuhudumia wakazi 27,000, lakini kwa sasa unahudumia zaidi ya wakazi 85,000 katika kata za Lamadi, Mkula na Lutubiga baada ya kupanua miundombinu ya usambazaji na kuongeza uwezo wa pampu, huku uzalishaji wa maji ukifikia lita milioni 33 kwa siku dhidi ya mahitaji ya lita milioni 24.2.
Kwa upande wa Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi unalenga kuhudumia wakazi wapatao 495,000 katika wilaya tano za Simiyu ambazo ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu. Unahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Bariadi, Busega, Itilima na vijiji 103, pamoja na miradi ya kilimo himilivu na uhifadhi wa mazingira unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2025.
Hii ni historia kwa Rais Samia kutekeleza hatua hizo mbili kubwa kwa Sekta ya Maji katika mkoa mmoja ndani ya siku moja, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.