Habari

Imewekwa: Jun, 17 2025

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Apongeza Utekelezaji wa Miradi ya Maji

News Images

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji madhubuti na wenye tija wa miradi ya majisafi na salama nchini, akisema kuwa mafanikio hayo yanadhihirika wazi kila inapopita mbio hizo na kukagua miradi ya maendeleo.

Ussi aliyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Mikocheni–Mkwaja, unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, chini ya usimamizi wa Wizara ya Maji.

“Wizara ya Maji imekuwa mstari wa mbele kutekeleza kwa ufanisi mkubwa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Utekelezaji huu si tu unaleta matumaini mapya kwa wananchi, bali pia ni heshima kubwa kwa Rais wetu ambaye ameonesha dhamira ya kweli ya kumtua mama ndoo kichwani,” Ussi amesema.

Ameongeza kuwa miradi mingi ya maji iliyokaguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi inaonesha mafanikio makubwa katika upatikanaji wa huduma za maji, hatua ambayo inachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi vijijini na mijini.

Naye Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na pia Mbunge wa Jimbo la Pangani, aliyehudhuria tukio hilo, amesisitiza kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha kuwa kila kijiji nchini kinafikiwa na huduma ya majisafi na salama kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Sekta ya Maji.

“Hatua tunazochukua sasa si za kawaida. Tunakwenda kuhakikisha hakuna Mtanzania anayesalia nyuma katika kupata huduma hii ya msingi. Mradi huu wa Mikocheni–Mkwaja ni miongoni mwa miradi mingi inayodhihirisha dhamira hiyo ya Serikali ya Awamu ya Sita. Tunapambana kuifikia Tanzania isiyo na kero ya maji,” Waziri Aweso amesema.

Aweso pia ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa katika hatua za utekelezaji wa miradi na kuahidi kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Mradi wa maji wa Mikocheni–Mkwaja unatekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa vijiji vinavyopitiwa na mradi huo katika Wilaya ya Pangani. Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutimiza azma ya kumtua mama ndoo kichwani.

Wananchi wa maeneo hayo wameeleza furaha yao na kusema kuwa ujio wa mradi huo utapunguza kwa kiwango kikubwa umbali waliokuwa wakiutembea kutafuta maji na pia kupunguza magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.