Habari
Serikali Kuanzisha Mamlaka ya Maji katika Mji Mdogo wa Lamadi

Simiyu; 08 Januari, 2020
TAARIFA KWA UMMA
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza ufanyike utaratibu wa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji kwa Mji wa Lamadi katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu itakayosimamia utoaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa mji huo na kumaliza kabisa kero za wananchi.
Mhe. Aweso ametoa maelekezo hayo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira wa mji mdogo wa Lamadi wenye thamani ya Shilingi bilioni 12.83 unaofanywa na Mkandarasi-M/S China Civil Engineering Construction Corporation chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
Naibu Waziri Aweso amebaini changamoto za uendeshaji na usimamizi wa mradi na kiufundi kwenye utekelezaji zilizosababisha malalamiko kwa wananchi, pamoja na mradi huo kuwa kwenye hatua ya matazamio ya kipindi cha mwaka mmoja kabla kukabidhiwa kwa wananchi.
Hatua iliyomlazimu kuvunja uongozi wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Busega kwa usimamizi mbovu na kutaka iundwe kamati itakayosimamia mradi kwa muda, wakati timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maji ikifanya utaratibu wa uanzishwaji wa mamlaka na kupitia mapungufu yote ya mradi.
Huku akimtaka mkandarasi kurekebisha mapungufu yote yatakayobainika kwa gharama zake kabla ya kuukabidhi, pamoja kufikisha huduma katika vijiji vyote vitatu vya Mwabayanda, Lamadi na Kalago vilivyopo katika Kata ya Lamadi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Aweso ameelekeza vyombo ya ulinzi na usalama kumkamata Mhandisi Mshauri-Kampuni ya Egis kwa kushindwa kusimamia ujenzi kikamilifu na kusababisha mapungufu kwenye mradi huo, pamoja Fundi Mchundo wa RUWASA katika Wilaya ya Busega kwa kosa la kuunganishia huduma wateja bila kufuata taratibu.
Awali, Naibu Waziri Aweso amempa wiki saba kuanzia 08 Januari, 2020 Mkandarasi RJR anayetekeleza ujenzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Nyamgana kukamilisha kazi hiyo.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini