Habari

Imewekwa: Jan, 05 2026

RUWASA Yachukua Hatua Kutatua Changamoto ya Upatikanaji wa Huduma ya Maji Kdete

News Images

Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umechukua hatua madhubuti kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Kata ya Kidete, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, baada ya timu ya wataalamu wake kuwasili katika kata hiyo kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina na kuchukua hatua za haraka.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maelekezo ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), aliyoyatoa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), iliyofanyika tarehe 2 Januari 2026 katika Kata ya Kidete, kufuatia kilio cha wananchi kuhusu upungufu wa huduma ya maji.

Timu hiyo ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mipango RUWASA, Enock Wagala, imehusisha wataalamu kutoka RUWASA Makao Makuu, Ofisi ya Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro pamoja na Ofisi ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilosa, imefanya tathmini ya hali halisi ya upatikanaji wa maji katika kata hiyo kwa lengo la kubaini suluhu za haraka na za kudumu kwa changamoto iliyodumu kwa muda mrefu.

Katika kikao cha pamoja na viongozi wa Serikali ya Kata pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kupitia Baraza la Maendeleo la Kata (BDC). Kikao hicho, kilichoongozwa na Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Kidete, kilijadili kwa kina changamoto ya upatikanaji wa maji, hali ya vyanzo vya maji vilivyopo pamoja na mahitaji halisi ya wananchi.

Wajumbe walikubaliana zichukuliwe hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuanza mara moja utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa visima vya maji. Aidha, iliazimiwa kuwa mitambo ya uchimbaji wa visima itawasili katika Kata ya Kidete kwa kuchimba visima viwili (2) mara moja katika Vijiji vya Kidete Kibaoni na Kitati.

Miradi hiyo ipo katika Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na itatekelezwa chini ya usimamizi wa RUWASA, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi, salama na ya uhakika.

Wananchi wa Kata ya Kidete wameeleza kuridhishwa na kufurahishwa kwao na hatua zilizochukuliwa na Serikali, wakionesha imani yao kwa RUWASA na dhamira ya Serikali katika kutatua changamoto ya maji kwa vitendo. Wananchi hao wameahidi kutoa ushirikiano wote unaohitajika ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa ya kudumu kwa jamii.