Habari

Imewekwa: Jan, 05 2026

Dkt. Nchemba Ataka Bwawa la Kidunda Kukamilika kwa Wakati

News Images

Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha mradi wa Bwawa la Kidunda unasimamiwa kwa karibu na unakamilika kwa wakati ili kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Dkt. Nchemba amesema kuwa mradi huu unakidhi maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukabiliana na changamoto za upungufu wa maji, hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, akitoa maelezo hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo.

Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha utekelezaji wa bwawa hilo unakamilika kwa wakati, huku miradi mingine mikubwa ya kimkakati ikiendelea, ikiwemo Mradi wa Miji 28, Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Visima 900, yote inaigharimu Serikali fedha nyingi kama hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto za wananchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Nchemba ameitaka Wizara ya Maji kuandaa bangokitita mahsusi kwa ajili ya mkandarasi ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema kuwa mradi huu, unaogharimu shilingi bilioni 366, utasaidia kuzalisha takriban lita bilioni 20 za maji kwa siku na megawati 20 za umeme, akziztaja kama sehemu ya manufaa ya bwawa hilo. Aidha, mradi huo utawezesha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 72.

Amesema kuwa Bwawa la Kidunda pia litahifadhi lita bilioni 190 za maji, ambazo zitasaidia matumizi ya nyumbani, hasa kipindi cha ukame pale kina cha mto Ruvu kinapopungua. Waziri Aweso amesisitiza kuwa mradi huu utatatua changamoto ya upungufu wa maji katika mikoa mitatu, hususan wakati wa kiangazi, wakati mikoa hiyo inakabiliwa na uhaba wa maji.