Habari

Imewekwa: Jan, 06 2026

Serikali Yajadiliana na Exim Bank India Kukamilisha Miradi ya Maji kwa Wakati

News Images

Serikali imefanya mazungumzo na kuhusu Mradi wa Kimkakati wa Miji 28 na Mwakilishi wa Benki ya Exim ya India kuzingatia makubaliano na kukamilisha ujenzi wa Mradi ya Maji wa Miji 28 na kuanza utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Tinde-Shelui – Awamu ya Pili ili kuondokana na changamoto ya huduma ya majisafi na salama.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Diana Kimaro amesema kuwa ni muhimu Benki ya Exim ya India kuzingatia mikataba ya utekelezaji iliyosainiwa kati yake na serikali ya tanzania wa miradi ya maji katika miji 24 iliyo chini ya ufadhili wake pamoja na kuanza kazi ya utekelezaji wa Mradi wa Tinde-Shelui awamu ya pili uliosimama kwa muda mrefu,

Ameyasema hayo wakati wa kikao kazi cha kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Miji 28 kilichofanyika makao makuu ya Wizara ya Maji, Mtumba jijini Dodoma.

Bi. Kimaro amesema kuwa licha ya maendeleo mazuri katika baadhi ya maeneo, nguvu zaidi zinatakiwa kuelekezwa katika miji ambayo utekelezaji wake bado uko chini, hususan Singida,Kihomboi na Chunya. Akisisitiza kuwa ni muhimu fedha zitoke kwa wakati na mkandarasi afanye kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kulingana na mkataba.

Mradi wa Kimkakati wa Miji 28 unagharimu takribani Sh. trilioni 1.58 ambapo takriban shilingi bilioni 400 zimetolewa na Serikali ya Tanzania, huku shilingi trilioni 1.18 zikitokana na mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ya India.

Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi zaidi ya milioni 67.9 na kwa sasa umefikia asilimia 55 ya utekelezaji wake.

Aidha, kikao hicho pia kimejadili kuendelea kwa utekelezaji wa Mradi wa Tinde–Shelu Awamu ya Pili na kutaka utekelezaji wake uwe umeanza ifikapo mwezi Juni mwaka huu ,Mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani dola za marekani milioni 6.9 ambazo ni bakaa ya fedha zilzookolewa kutoka Mradi wa Maji wa Tabora–Igunga–Nzega,

Ambapo kazi za ujenzi zitahusisha ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, na unatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 108,000 wa miji ya Tinde, Shelui na vijiji vya jirani 34.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Benki ya Exim, Ravi V. P. Singh, ameutambua mchango mkubwa wa Sekta ya Maji katika maendeleo ya nchini ya Tanzania pamoja na ushirikiano baina ya Exim Benki ya India na Sekta ya Maji Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya Serikali za Tanzania na India katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Lengo kuu la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya majisafi na salama ili kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji nchini.