Habari

Imewekwa: Sep, 15 2025

​RC Mara awataka waratibu Siku ya Mto Mara kuwashirikisha wadau zaidi

News Images

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amewataka waandaaji wa siku ya Bonde la Mto Mara kuongeza jitihaza katika kuwashirikisha wadau kutoka Tanzania, na Kenya pamoja na wadau wa mendeleo ili kufanikisha utunzaji wa Bonde la Mto Mara.

Wito huo ameutoa alipomwakilisha Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika kufunga maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mara yaliyofanyika mjini Butiama.

Amesema bonde la mto Mara lina umuhimu mkubwa kwa jamii ya Tanzania na Kenya inayozunguka bonde hilo hivyo njia mbalimbali zinatakiwa kutumika ili kufikia malengo.

Amepongeza jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika zimesaidia kuendelea kuwepo kwa bonde hilo ambalo matokeo yake ni mto Mara ambao umechangia kuifanya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa moja ya Maajabu Saba ya Dunia.

Amesema jitihada hizo pia zilenge kuwa na Jukwaa la wadau wa Mto Mara na kufufua Jukwaa la Jumuia ya Watumia Maji ambalo linaweza kuweka utaratibu wa kukutana angalau mara mbili kwa mwaka.

Amepongeza jitihada zinazoendelea ikiwemo kuanzisha mpango wa pamoja wa matumizi ya maji pamoja na hati ya makubaliano kuhusu usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ya Mto Mara.

Amesisitiza uanzishaji wa vikundi vya uhifadhi wa mazingira shuleni ili kuwajengea uelewa na utayari wa kulinda mazingira kuanzia ngazi ya shule.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ametoa salamu za Wizara ya Maji akieleza kuwa imeridhishwa na ushiriki wa wadau katika maadhimisho na imetumia fursa ya maadhimisho kufanya ukaguzi wa miradi ya maji ya Mugango-Kiabakari-Butiama, Mugumu-Seregenti na mradi wa maji wa Tarime-Rorya inayotekelezwa na Wizara ya Maji mkoani Mara.

Amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mara kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mkoani hapo na anaendelea na jithada kuhakikisha lengo la "kumtua mama ndoo ya maji kichwani" linafanikiwa