Habari
Serikali Kuimarisha Ushirikiano na Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo katika Utoaji wa Huduma
Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira, kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Akifungua Warsha ya Uhakiki na Ujenzi wa Uwezo iliyofanyika katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bw. Henry Chisute, amesema Serikali imedhamiria kuimarisha mifumo shirikishi ili kuhakikisha huduma bora na endelevu zinawafikia wananchi.
Amesema Tanzania imepiga hatua nzuri katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira, hali inayoonesha mafanikio ya juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Hata hivyo, amesema ongezeko la idadi ya watu, kasi ya ukuaji wa miji, pamoja na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kuongeza shinikizo katika mifumo ya maji na usafi wa mazingira. Hivyo, kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha na kuimarisha mbinu za utoaji wa huduma ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi.
Bw. Chisute amebainisha kuwa jitihada za Serikali pekee hazitoshi kufikia ukubwa wa malengo yaliyowekwa, hivyo ni muhimu kwa sekta binafsi kushiriki kwa nguvu zaidi, kwa mpangilio mzuri na kwa ubunifu, katika utoaji wa huduma, uwekezaji na kuhakikisha uendelevu wa miradi ya maji na usafi wa mazingira.
Ameongeza kuwa lengo la Serikali si kuhamisha jukumu kutoka kwa taasisi za umma, bali ni kujenga mfumo imara na shirikishi zaidi unaowezesha wadau wa umma na binafsi kushirikiana kikamilifu katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira.
Warsha hiyo imehudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi, pamoja na washirika wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, UNICEF, GIZ, AFD na KfW.

