Habari
Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Utendaji wa RUWASA na Mfuko wa Maji
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeeleza kuridhishwa na utendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji, hususan Mfuko wa Taifa wa Maji na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kutokana na utekelezaji wenye weledi wa miradi ya maji nchini.
Kamati hiyo imepongeza mwelekeo wa utekelezaji wa miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, ikibainisha kuwa juhudi zinazofanywa na taasisi hizo zinaendana na malengo ya Serikali ya kuboresha ustawi wa jamii.
Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Prof. Pius Yanda (Mb), alisema Kamati imepokea na kujadili taarifa za utekelezaji zilizowasilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Maji, Wakili Haji Nandule, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta Kirita, kwa niaba ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb).
Kamati hiyo imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali fedha, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji, pamoja na kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwapatia wananchi huduma ya maji endelevu, salama na ya uhakika.

