Habari
IGUWASA Yawekeza Zaidi ya Sh. Bilioni 1.86 Kwenye Huduma ya Usafi wa Mazingira

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) imeanza kutumia magari mapya ya kisasa ya uondoshaji majitaka, baada ya uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 1.86 katika mradi wa ujenzi wa mabwawa ya majitaka na ununuzi wa magari hayo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi magari mapya mjini Igunga, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Sauda Mtondoo, amesema kuwa huduma ya uondoshaji majitaka ni nguzo muhimu ya usafi wa mazingira na afya ya jamii. Akifafanua kuwa bila mifumo bora ya majitaka, wananchi wako hatarini kupata magonjwa ya milipuko na uharibifu wa mazingira.
“Magari haya ya kisasa yatumike vizuri kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majitaka haraka, bora na kwa gharama nafuu. Ni imani yangu kuwa hatua hii itasaidia kupunguza hatari za magonjwa ya milipuko na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla,” Mhe. Mtondoo amesisitiza.
Aidha, Mhe. Mtondoo ametoa pongezi kwa IGUWASA kwa kuanza kutumia magari haya, akisema hatua hii inaendana na kasi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita, katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za msingi za maji na usafi wa mazingira.
Magari haya yamepatikana kupitia Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Majitaka, unaotekelezwa na Mkandarasi Peritus Exim Private Ltd, chini ya usimamizi wa IGUWASA kwa kushirikiana na Serikali Kuu na wadau wa maendeleo. Mradi huu wenye thamani ya Sh. bilioni 1.86 unalenga kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, utibuji, na usafishaji wa majitaka kwa njia salama na endelevu. Mpaka sasa, mradi umefikia asilimia 48 na utekelezaji wake unaendelea.
Katika hafla hiyo, Mhe. Mtondoo pia amezindua Mkataba wa Huduma kwa Mteja, unaolenga kuimarisha uwajibikaji na uwazi kati ya mamlaka na wateja wake. Alisisitiza IGUWASA kuhakikisha wateja wanapata taarifa kamili kuhusu viwango vya huduma, malalamiko yao yanashughulikiwa kwa wakati, na mawasiliano kati ya wateja na mamlaka yanaimarishwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa IGUWASA, Alex Ntonge, amesema kuwa kupitia mkataba huu, wateja watafahamu viwango vya huduma wanavyostahili kupokea. Pia, mkataba huo utatoa mwongozo kwa IGUWASA kuhakikisha wateja hawapati usumbufu, na changamoto, malalamiko na maoni ya wateja yanashughulikiwa kwa wakati.
Hii ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira, na inathibitisha jitihada za IGUWASA kuhakikisha jamii inapata huduma bora.