Habari

Imewekwa: May, 21 2025

Sekta ya Maji Yazidi Kuimarika Kupitia Ushirikiano na Wadau wa Kimataifa

News Images

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa kimataifa katika juhudi za kuharakisha maendeleo ya Sekta ya Maji na kuhakikisha huduma bora zaidi kwa wananchi.

Wizara ya Maji imekutana na ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na Asasi ya Kimataifa ya WaterAid kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi.

Kikao hicho muhimu kimefanyika jijini Dodoma kikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, pamoja na Menejimenti ya Wizara. Mazungumzo yamejikita katika kutathmini hatua zilizofikiwa, changamoto zilizopo, na fursa za kuimarisha zaidi utekelezaji wa miradi ya maji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Kikao hiki kimefanyika takribani miezi miwili tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutunukiwa Tuzo ya Kinara wa Maji Afrika (Pan-African Water, Sanitation and Hygiene Award) na WaterAid kama kutambua uongozi wake mahiri katika kusimamia maboresho ya huduma za maji na usafi wa mazingira nchini. Kupitia tuzo hiyo, Rais Samia pia alipewa heshima ya kuwa Mlezi wa Bara la Afrika katika Masuala ya Maji na Usafi wa Mazingira – hatua inayoakisi heshima na ushawishi mkubwa wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa ya sekta ya maji.

Aidha, katika maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani tarehe 22 Machi 2025, Rais Dkt. Samia alitunukiwa Tuzo ya Kitaifa ya Mageuzi katika Sekta ya Maji (Game Changer Award), kutokana na mchango wake mkubwa katika kuleta mageuzi ya kimkakati ndani ya sekta hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Gemma Querol Prades, Kiongozi Mkuu wa Idara ya Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi kutoka UNICEF, amesema Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya maji, na kwamba UNICEF itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania ili kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana, hususan katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu za maji safi na salama kwa Watanzania wote.

Ushirikiano huu unaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania ya kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kujenga taifa lenye huduma bora za maji na usafi wa mazingira, kwa ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya taifa.