Habari
Serikali Yajizatiti Kutunza Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Taifa

Serikali kupitia Wizara ya Maji inaendelea kuongeza kasi ya juhudi za kutunza na kulinda vyanzo vya maji nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha usalama wa maji kwa matumizi ya sasa na kwa vizazi vijavyo.
Juhudi hizi zinaendana na dhamira ya Serikali ya kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wote kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday ameongoza majadiliano ya kitaalamu kuhusu uendelezaji wa rasilimali maji nchini, katika kikao kazi kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji, Jijini Dodoma. Majadiliano hayo ya siku mbili yanalenga kuibua mikakati bunifu ya kuhakikisha ulinzi, usimamizi madhubuti na matumizi endelevu ya vyanzo vya maji nchini.
Kikao kazi hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji wakiwemo Washirika wa Maendeleo, Taasisi za Serikali, Wataalamu wa Sekta ya Maji pamoja na wawakilishi kutoka Sekta Binafsi. Ushirikiano huu unalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu changamoto zilizopo na fursa zinazopatikana katika usimamizi wa rasilimali maji, hasa katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na mahitaji yanayoongezeka ya maji kwa ajili ya kilimo, viwanda na matumizi ya nyumbani.
Miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa ni pamoja na namna bora ya kusimamia na kufuatilia fedha zinazotolewa kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa rasilimali maji, kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maji, pamoja na kuhakikisha ubora wa maji unaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.
Katika kikao hicho Mkurugenzi Sunday amesisitiza kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji si jukumu la Serikali pekee bali ni wajibu wa kila mwananchi. Ameongeza kuwa mafanikio ya Sekta ya Maji yanategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wadau wote na uwekezaji wa kimkakati katika uhifadhi wa mazingira na teknolojia rafiki za uhifadhi wa maji.
Serikali imekuwa ikiweka msukumo mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kisheria, kitaasisi na kimkakati inayosimamia rasilimali maji; ikiwa ni pamoja na kuboresha sera na kanuni, kuanzisha maeneo tengefu ya vyanzo vya maji na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Kwa ujumla, majadiliano hayo yanatoa jukwaa muhimu kwa Serikali na wadau wake kujipanga kikamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba Sekta ya Maji, huku yakilenga kuleta mabadiliko chanya kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa kupitia usimamizi bora wa rasilimali maji.