Habari
Wizara ya Maji kuja na gridi ya Taifa ya maji bora zaidi Afrika Mashariki na Kati
Tanzania inaendelea na mpango wa ujenzi wa gridi ya taifa ya maji ambao kukamilika kwake kutaifanya kuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwa na Gridi ya uhakika na yenye mtandao imara wa maji. Mpango huu unahusisha matumzi ya maji kutoka vyanzo vya uhakika ikiwemo mito na maziwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew katika ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) akiwa katika mji mdogo wa Laela Wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Amesema mpango huu ni wa uhakika kutokana na dhamila ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan ambaye ameonesha uthubutu katika maeneo mengi ya sekta ya maji tangu ameingia madarakani.
Ametolea mfano kuwa wakati mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani kwa mara ya kwanza bajeti ya Wizara ya Maji ilikuwa shilingi bilioni 680 lakini bajeti ya maji kwa mwaka 2025/2026 bajeti ya Wizara ya Maji ilifikia shilingi tlilioni 1.01.
Amesema tayari serikali kupitia Wizara ya Maji imeanza upembuzi yakinifu katika ziwa Tanganyika ili kuwezesha maji kutoka ziwa hilo kuhudumia mikoa ya Kigoma, Songwe, Katavi na Rukwa huku dhamira hiyo ikiendelea ili kuvifikia vyanzo vyote vya uhakika vya maji katika mikoa mbalimbali nchini.
Aidha, amezungumzia huduma ya maji katika mkoa wa Rukwa kuwa serikali imetoa takribani shilingi bilioni 49 ambazo zimetekeleza miradi ya maji 82 huku Sumbawanga pekee ikiwa imetekeleza na kukamilisha miradi 17 yenye thamani ya shilingi bilioni 6, miradi 16 yenye gharama ya zaidi ya shilinig bilioni 16 ikiwa inaendelea.
Amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwa ushirikiano mkubwa mbao wamekuwa wakiutoa na kuwaahidi kuhakikisha malengo yote yaliyokusudiwa ya kufikisha huduma ya maji kwa asilimia mia moja yanakamilika.

