Habari
Wataalamu wa Sekta ya Maji Wapatiwa Mafunzo ya Kuimarisha Usimamizi wa Ubora wa Maji katika Mabwawa Madogo
Wataalamu kutoka Sekta ya Maji wamepatiwa mafunzo maalumu yenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna bora ya kuandaa mpango wa kutathmini na kufuatilia ubora wa maji katika mabwawa madogo nchini kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mifugo, kilimo na matumizi ya nyumbani.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, hususan katika vyanzo vya maji visivyo rasmi, pamoja na kuhakikisha maji yanayotumika na jamii yanakuwa salama na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya watumiaji.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Jijini Dodoma yamelenga pia kuboresha uelewa wa wataalamu kuhusu usanifu, uendeshaji, usimamizi na uendelevu wa mabwawa madogo, pamoja na kuendeleza mbinu bora za usimamizi wa vyanzo vingine vya maji vinavyotumiwa na jamii katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, wataalamu wameeleza kuwa mabwawa madogo yana mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi, hasa katika maeneo ya vijijini ambako jamii hutegemea zaidi vyanzo hivyo kwa ajili ya uzalishaji na matumizi ya kila siku.
Aidha, mafunzo hayo yanahusisha namna ya kupima, kuchambua na kutathmini ubora na usalama wa maji yanayotumika katika shughuli za kibinadamu, ikiwemo matumizi ya nyumbani, shughuli za mifugo, kilimo na shughuli nyingine za kijamii. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa jamii zinapata maji salama yanayolinda afya zao na kuongeza tija katika shughuli zao za uzalishaji.
Juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji nchini kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali za maji. Mafunzo hayo pia yanakwenda sambamba na Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, Toleo la 2025, ambayo inalenga kuimarisha upatikanaji wa maji, hususan katika maeneo ya vijijini, pamoja na kuhakikisha juhudi za kufikisha huduma za maji katika vijiji vilivyosalia zinafanikiwa ifikapo mwaka 2030.
Katika kutekeleza malengo hayo, Serikali imeendelea kushirikiana na taasisi za utafiti za ndani na kimataifa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuendeleza ubunifu wa kiteknolojia, tafiti na mbinu bora za usimamizi wa mabwawa madogo na vyanzo vingine vya maji.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza uwezo wa kitaalamu, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa ubora wa maji na kuhakikisha maamuzi yanayofanyika katika usimamizi wa rasilimali za maji yanazingatia ushahidi wa kitaalamu na mahitaji halisi ya jamii.
Mtaalamu wa Ubora wa Maji, Profesa Kenneth Irvine kutoka Chuo Kikuu cha Elimu ya Maji cha IHE Delft nchini Uholanzi, ndiye aliyetoa mafunzo hayo kwa wataalamu wa Sekta ya Maji. Kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata maarifa na uzoefu wa kimataifa kuhusu namna ya kuimarisha mifumo ya tathmini ya ubora wa maji, usimamizi wa mabwawa madogo na matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza umuhimu wa kuendelea kujengewa uwezo wataalamu wa sekta ili waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika usimamizi wa maji, ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la mahitaji ya maji na uharibifu wa baadhi ya vyanzo vya maji.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mabwawa madogo na kusaidia kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika sekta ya maji unaleta manufaa makubwa kwa wananchi, hususan wale wanaoishi katika maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa maji.

