Habari

Imewekwa: Jul, 17 2026

​Mkutano wa nane wa SADC wa Maji Chini ya Ardhi Kufanyika Tanzania.

News Images

Taasisi ya Usimamizi wa Maji Chini ya Ardhi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-GMI), kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na wadau mbalimbali wa kikanda na kimataifa wanashirikiana kuandaa Mkutano wa nane wa SADC wa Maji Chini ya Ardhi, utakaowakutanisha wataalamu, watunga Sera na wadau wengine ili kuimarisha usimamizi endelevu wa maji chini ya ardhi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo, "Vyanzo vya Maji Chini ya Ardhi Vinavyoshirikishwa, Sauti Sawa: Kuharakisha Uhimilivu wa Maji Chini ya Ardhi kwa Mustakabali Salama wa Maji," .

Mkutano utakuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa, ubunifu na uzoefu katika usimamizi wa maji chini ya ardhi, ukiweka msisitizo katika usimamizi endelevu wa vyanzo vya maji chini ya ardhi vinavyovuka mipaka ya nchi.

Lengo la mkutano ni kuhimiza kubadilishana mbinu bora, matokeo ya tafiti na uzoefu wa kitaalamu katika maendeleo na usimamizi wa maji chini ya ardhi, sambamba na kujadili changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta hiyo.

Aidha, mkutano utaonesha mchango mkubwa wa maji chini ya ardhi katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kuimarisha usalama wa maji katika nchi wanachama wa SADC.

Washiriki wa mkutano huo watakuwa viongozi wa serikali, taasisi za kikanda, washirika wa maendeleo, viongozi kutoka sekta binafsi, watafiti, wasomi, wanasayansi, na AZAKI.

Aidha, wadau wote wanakaribishwa wenye nia ya kushiriki kama wawasilishaji wa mada au washiriki wa kawaida, kwakuwa mkutano huo utatoa fursa ya kipekee ya kuimarisha ushirikiano, kuhamasisha ubunifu na kuharakisha juhudi za pamoja za kuhakikisha usimamizi endelevu na wenye ustahimilivu wa maji chini ya ardhi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa maelezo ya kina kuhusu usajili, mwongozo wa uwasilishaji wa mada na muhtasari, pamoja na taarifa za maandalizi na uratibu wa mkutano, tafadhali tembelea tovuti ya SADC-GMI,

www.sadc-gmi.org.


Kitengo cha Mawasiliano