Habari

Imewekwa: Nov, 28 2025

​Wahitimu wa Chuo cha Maji Wapate Nafasi Kwenye Sekta ya Maji – Aweso

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezitaka taasisi za Sekta ya Maji kuwapa nafasi vijana ambao ni wahitimu wa fani mbalimbali katika Chuo cha Maji kuonyesha ujuzi wao.

Amesema hatua hiyo itaimarisha utekelezaji, uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maji mijini na vijijini.

Waziri Aweso akiongea katika sherehe ya mahafali ya 49 ya Chuo cha Maji jijini Dar es Salaam, amesema wataalam hao watumike kama nguvu kazi itakayoimarisha na kuongeza ufanisi wa utendaji.

“Tunazo taasisi mbalimbali kwenye sekta yetu kama Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka za Maji, Bodi za Maji za Mabonde. Tufuate taratibu za utumishi vijana hawa wapewe mikataba ya kazi watusaidie kwenye maeneo mbalimbali”, Aweso amesema.

“Wahitimu hawa watumike kuimarisha utendaji wa shughuli mbalimbali, kutatua changamoto na kuongeza tija kwenye sekta yetu”, Aweso amesisitiza.

Waziri Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji haitawaacha wataalam hao na kuahidi kuwa wahitimu waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo yao, watapewa nafasi za kuonyesha uwezo kikazi pamoja na ufadhili wa ngazi nyingine kimasomo.

Pia, ametoa rai kwa wahitimu hao kuwa wajasiri na wabunifu kuzitumia changamoto katika Sekta ya Maji kama fursa.

Amekitaka Chuo cha Maji kujikita katika kufanya tafiti za kina zenye kutoa majibu na suluhisho za changamoto mbalimbali za Sekta ya Maji ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa maji na ufanisi wa matumizi ya dira za maji za kabla ya matumizi (pre-paid meters).

Waziri Aweso ameweka bayana dhamira yake ya kuzidi kukiimarisha chuo hicho kwa lengo la kuwa miongoni mwa vyuo bora Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi kutoka nchi zote duniani.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezindua rasmi bodi mpya ya Chuo cha Maji ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Maulid Maulid, na kuitaka bodi hiyo kushauri ipasavyo, kusimamia utendaji wa menejimenti kwa karibu na kukipeleka chuo katika hatua nyingine.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ametoa rai kwa Chuo cha Maji kuzalisha wataalam kwenye Kada ya Ufundi Sanifu kwa kuwa ndiyo wanaotumika kufanya kazi nyingi kwenye ujenzi na uendeshaji wa miradi ya maji.

Mhandisi Mwajuma ametoa rai hiyo mara baada ya kubaini uchache wa Mafundi Sanifu waliohitimu, ambao walikuwa 17 pekee ukilinganisha na idadi ya wahitimu wa fani nyingine.

Jumla ya wahitimu 881 wa fani mbalimbali katika ngazi za Cheti, Astashahada, Astashahada ya Juu, Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamili wamehitimu ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 28 ukilinganisha na mwaka uliopita.

Kitengo cha Mawasiliano