Habari

Imewekwa: Jul, 16 2026

Serikali Yasaini Ruzuku ya Sh. Bil 60.7 Na Ujerumani Kuboresha Huduma ya Maji Tunduma na Vwawa–Mlowo

News Images

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa ruzuku na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani wenye thamani ya Euro milioni 20, sawa na takribani shilingi bilioni 60.7, kwa ajili ya kuboresha huduma za maji katika miji ya Tunduma na Vwawa–Mlowo.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha, jijini Dodoma. Kupitia makubaliano hayo, Tanzania itanufaika na ruzuku inayotolewa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani katika kuchochea maendeleo endelevu, hususan katika sekta ya maji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ameishukuru Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha sekta ya maji na kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji katika huduma za maji safi na salama.

Mhandisi Waziri amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utachangia kuimarisha miundombinu ya maji na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji unaozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, mradi huo utaboresha upatikanaji wa huduma za maji safi, salama na za uhakika kwa wananchi wa Tunduma na Vwawa–Mlowo, huku ukiongeza uwezo wa mifumo ya maji kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.

Ameeleza kuwa upatikanaji wa huduma bora za maji ni msingi muhimu wa kuboresha afya za wananchi, kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji, kuimarisha huduma za elimu na afya, pamoja na kupunguza muda unaotumiwa kutafuta maji, hususan kwa wanawake na watoto. Vilevile, mradi huo unatarajiwa kuboresha huduma za usafi wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Mkakati huu unaendana kikamilifu na vipaumbele vya maendeleo vya Serikali, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Maji, pamoja na dhamira ya Tanzania ya kufikia Lengo la Sita la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 6), linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira kwa wote," amesema Mhandisi Waziri.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Ruzuku hiyo inaonesha dhamira ya pamoja ya pande hizo mbili ya kuwekeza katika miundombinu endelevu, kuimarisha ustawi wa jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi unaojumuisha wananchi wote.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira, kuboresha afya na ustawi wa wananchi, kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika miji ya Tunduma na Vwawa–Mlowo, na kuchangia azma ya Serikali ya kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa usawa, kwa ubora na kwa uendelevu kwa Watanzania wote.