Habari
Simiyu: Utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Wafikia Asilimia 72
Utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika Mkoa wa Simiyu umefikia wastani wa asilimia 72, huku wadau wakikutana kujadili maendeleo ya utekelezaji wake na hatua zinazofuata ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Kikao kazi hicho kimeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bi. Rose Ambrose, na kimehusisha wadau mbalimbali wa serikali kujadili mwenendo wa mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund – GCF) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mratibu wa Mradi, Mhandisi Annastazia Bulogo, amesema kuwa hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 71.8, na kwamba unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi Bilioni 440 za Kitanzania hadi kukamilika kwake.
Ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2027, na utaendelea kuchangia juhudi za taifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan katika kuboresha upatikanaji wa maji na kuimarisha ustahimilivu wa jamii katika maeneo yanayoathiriwa na ukame na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Bi. Rose Ambrose amekihakikishia kikao hicho kuwa Wizara ya Maji inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kukamilika kwa wakati licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.
Amesema wizara itaendelea kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto zote zilizojitokeza na zile zitakazojitokeza ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa wakati uliopangwa.
Aidha, amemtaka Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Annastazia Bulogo, kukutana na wadau kutoka wizara mbalimbali za kisekta ili kujadili na kupata suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazoweza kuathiri utekelezaji wa mradi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Wadau hao wamejadili masuala mbalimbali ya utekelezaji na uratibu wa mradi huo.
Imeelezwa kuwa kikao kingine cha tathmini ya maendeleo ya mradi kinatarajiwa kufanyika tena mwezi Agosti 2026 ili kuendelea kufuatilia hatua za utekelezaji wake.

