Habari
Wataalam wa RUWASA Wanolewa Kuandaa Mipango Kabambe ya Maji na Usafi wa Mazingira
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kwa kushirikiana na Shirika la Water for People Tanzania, umeendesha mafunzo maalum kwa wataalam wanaounda Timu ya Uandaaji wa Mipango Kabambe ya Maji na Usafi wa Mazingira kutoka mikoa yote nchini, ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa zoezi hilo katika wilaya zote za Tanzania.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni mjini Morogoro, yamewakutanisha jumla ya wataalamu 85 kutoka Makao Makuu ya RUWASA, Ofisi za Sekretarieti za Tawala za Mikoa (RAS), pamoja na ofisi za RUWASA ngazi ya mkoa. Washiriki wamepatiwa ujuzi na mbinu za kitaalamu zitakazowawezesha kuandaa mipango kabambe yenye ubora, inayozingatia mahitaji halisi ya wananchi pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kuweka msingi imara wa utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Maji na Usafi wa Mazingira katika wilaya zote nchini, zoezi ambalo linatarajiwa kuanza rasmi katika mwaka wa fedha 2026/27. Mipango hiyo itakuwa nyenzo muhimu katika kuongoza uwekezaji, ujenzi na usimamizi wa miradi ya maji na usafi wa mazingira kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta Kirita, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mbaraka Ally, aliwataka washiriki kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kuongeza ujuzi na kuandaa mipango yenye ubora itakayowezesha utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira kwa ufanisi katika wilaya zote nchini.
Alisisitiza kuwa Mipango Kabambe itasaidia kubaini mahitaji ya huduma za maji na usafi wa mazingira katika kila eneo, kupanga vipaumbele vya uwekezaji, kuimarisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo na kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa endelevu na yenye tija kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Water for People Tanzania, Dkt. Happiness Willbroad, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uwezo wa ndani wa wataalamu wa Tanzania katika kupanga, kusimamia na kutekeleza miradi endelevu ya maji na usafi wa mazingira. Alieleza kuwa ushirikiano kati ya Water for People Tanzania na RUWASA unaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wote wa vijijini wanapata huduma za maji safi, salama na za uhakika.
Katika kipindi chote cha mafunzo, washiriki walijadili na kuoanisha hatua mbalimbali za kiufundi zinazohitajika katika uandaaji wa Mipango Kabambe, ikiwa ni pamoja na mbinu za ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu, upangaji wa vipaumbele vya uwekezaji, pamoja na uandaaji wa mikakati ya utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi. Aidha, waliandaa mkakati wa pamoja utakaohakikisha zoezi la kuandaa mipango hiyo linatekelezwa kwa wakati, kwa viwango vinavyokubalika na kwa ufanisi mkubwa.
Utekelezaji wa Mipango Kabambe ya Maji na Usafi wa Mazingira unatarajiwa kuimarisha upangaji wa sekta ya maji nchini, kuongeza ufanisi wa uwekezaji katika miradi ya maendeleo, kuboresha upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi wa vijijini, na kuwezesha RUWASA kupata msingi imara wa kupanga, kutekeleza na kusimamia miradi yenye tija na uendelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

