Habari
Kazi ya Kurejesha Njia ya Asili ya Mto Ruvu Yaendelea Vizuri
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amekagua kazi ya kurejesha Mto Ruvu katika njia yake ya asili katika Kijiji cha Kitomondo, Mkoa wa Pwani, kazi inayolenga kuzuia upotevu wa maji uliokuwa ukitokea kutokana na mto huo kuacha mkondo wake wa awali.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za Sekta ya Maji katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa huduma ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Akizungumzia utekelezaji wa kazi hiyo, Mhe. Aweso ameipongeza Bodi ya Maji ya Bonde la Wami–Ruvu kwa kazi kubwa iliyofanyika hadi sasa ya kuurejesha mto katika mkondo wake wa asili, hatua iliyosaidia kuongeza kiasi cha maji kinachofika katika mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.
“Nimejionea kazi inayoendelea na kwa dhati nimeridhishwa. Inanipa imani kubwa kuwa tutavuka salama katika kipindi hiki cha mpito. Nawapongeza Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), vyombo vya ulinzi na usalama vya mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam pamoja na wadau wote wanaoshiriki katika kazi hii kuhakikisha inakamilika kwa wakati,” Aweso amesema.
Ameeleza kuwa maendeleo ya kazi hiyo ni hatua muhimu katika jitihada za kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam na Pwani wanapata huduma endelevu ya maji, huku akiendelea kutoa wito kwa wananchi kutumia maji kwa uangalifu na kujenga utamaduni wa kuyahifadhi pale yanapopatikana.
Aidha, Waziri Aweso amesema Serikali imepokea taarifa njema kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuwa mvua zinaanza kunyesha, na tayari baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro yameshapata mvua. Ameeleza kuwa ana imani kubwa kipindi hiki cha mpito kitapita salama na hali ya upatikanaji wa maji kurejea katika hali ya kawaida.
“Katika kipindi hiki, Serikali itaendelea kuhakikisha maji yanayopatikana yanagawanywa kwa usawa kwa wananchi wote,” Aweso amesisitiza.

