Habari
Waziri Mkuu Dkt. Nchemba Aipongeza Sekta ya Maji
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Maji wa Lindi–Ruangwa–Nachingwea wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 119 katika kijiji cha Chimbila A, wilayani Ruangwa mkoani Lindi, na kuipongeza Sekta ya Maji pamoja na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika nchini.
Dkt. Nchemba ameonesha kuridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi huo, huku akiipongeza Sekta ya Maji kwa mafanikio makubwa katika kuboresha huduma za maji mijini na vijijini. Kipekee, amempongeza Waziri Aweso, kwa uongozi madhubuti na usimamizi wenye ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.
Mradi huo mkubwa wa maji, unaochota maji kutoka Mto Nyangao uliopo Wilaya ya Lindi, unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Mradi huo unatarajiwa kunufaisha jumla ya vijiji 56, ikiwemo vijiji 34 vya Wilaya ya Ruangwa, vijiji 21 vya Wilaya ya Nachingwea na kijiji kimoja cha Wilaya ya Lindi.
Hadi sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 67. Mradi ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Februari 2023 na unatarajiwa kukamilika Juni 2026 kwa awamu ya kwanza. Aidha, ifikapo Februari 2026, baadhi ya vijiji vitakuwa vimeanza kupata huduma ya majisafi na salama.
“Hiki ndicho ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka kuona utekelezaji wa kazi wenye ufanisi na tija. Hapa tumeona kiwango cha utekelezaji wa mradi kikiwa kikubwa kuliko fedha zilizokwisha kutolewa hadi sasa.” Dkt. Nchemba amesema katika hafla hiyo.
Aidha, ametumia muktadha huo kumpongeza aliyekuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa kuasisi mradi huo na kuhakikisha upatikanaji wa fedha zake katika kipindi chote cha utekelezaji.
Sekta ya Maji imeendelea kufanya vizuri ambapo Serikali imefanikiwa kukamilisha miradi 2,331 ya maji kati ya hiyo 1,965 vijijini na 366 mijini ambapo kukamilika kwa miradi hivyo kumeboresha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 83 na maeneo ya mijini kutoka wastani wa asilimia 84 hadi asilimia 91.6 kufikia Desemba 2024.

