Habari
Serikali Yajizatiti Kumaliza Changamoto ya Maji Dar
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema Serikali imejipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani, hali iliyosababishwa na kupungua kwa maji katika chanzo cha Mto Ruvu.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mhe. Aweso amesema Wizara ya Maji inaendelea kutekeleza mikakati ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa lengo la kuimarisha huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani, maeneo yaliyoathiriwa na ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Aweso amesema mikakati hiyo ni pamoja na kupunguza upotevu wa maji (Non-Revenue Water), kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, kujenga mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji kwa matumizi ya kipindi cha ukame, kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya maji.
Akifafanua zaidi, Mhe. Aweso amesema ujenzi wa Bwawa la Kidunda umefikia asilimia 40, mradi ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Gridi ya Maji ya Taifa inayolenga kutumia vyanzo vikubwa vya maji vilivyopo nchini, ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Mto Rufiji na vingine, ili kufikisha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa Dar es Salaam, Waziri Aweso amesema Serikali imeanza kutekeleza mikakati ya muda mfupi kwa kuchimba visima vipya vitano pamoja na kufufua visima vya zamani ili kuongeza upatikanaji wa maji. Kwa muda mrefu, Serikali inalenga kukamilisha Bwawa la Kidunda ifikapo mwezi Oktoba 2025, bwawa litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kiasi cha lita bilioni 190 na kutumia maji ya Mto Rufiji ili kuongeza uzalishaji wa maji.
Ameeleza kuwa mahitaji ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kwa ujumla sasa ni takribani lita 700,000 kwa siku, ambapo Dar es Salaam pekee ni takribani lita 534,000 kwa siku.
Waziri Aweso amesisitiza kuwa Mradi wa Bwawa la Kidunda ni wa kimkakati, kwani unatarajiwa kuzalisha lita bilioni 20 za maji kwa siku na utawezesha kukidhi mahitaji ya maji kwa idadi ya watu inayotarajiwa kufikia 11,387,753 ifikapo mwaka 2032, ambapo mahitaji ya maji yanakadiriwa kuongezeka na kufikia zaidi ya lita bilioni 1.028 kwa siku.
Amewasihi wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito, akieleza kuwa huduma ya maji itaendelea kuimarika kadri Serikali inavyoendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kudhibiti changamoto hiyo. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi maji na kuyatumia kwa uangalifu.
Vilevile, amewataka watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja kwa kusikiliza na kutatua kero zao kwa wakati, huku akisisitiza kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Amesema ni marufuku kwa watendaji wa Sekta ya Maji kuzoea kero za wananchi, akihimiza kuthamini wateja na kuwapatia huduma bora wanayostahili.
Katika kuhakikisha changamoto ya upungufu wa maji inapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Waziri Aweso amekuwa akifanya ziara mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, tangu mwezi Novemba 2025, ambapo wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali ya jiji na kuchukua hatua stahiki.

