Habari
Bwawa la Farkwa: Mradi wa Kimkakati wa Huduma ya Maji Wasaini Mkataba wa Ujenzi
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema kuwa ujenzi wa Bwawa la Farkwa ni mpango mkakati wa Serikali wenye lengo la kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma na maeneo yanayolizunguka.
Ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa Bwawa la Farkwa iliyofanyika katika Kijiji cha Bubutole, Kata ya Farkwa, Wilaya ya Chemba, Mkoa wa Dodoma.
Waziri Aweso ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kugharimu Shilingi bilioni 163.43 hadi kukamilika kwake na utakuwa na mchango mkubwa katika kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji Jijini Dodoma, kutokana na kuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 400 za maji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa kuu lenye urefu wa mita 1,300 na kimo cha mita 32, pamoja na bwawa saidizi lenye urefu wa mita 1,600 na kimo cha mita 15 kwa ajili ya kupunguza upotevu wa maji.
Baada ya kukamilika, bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kutoa mita za ujazo 7,236 za maji kwa siku. Aidha, mradi huo utahusisha ujenzi wa mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 128,000 za maji yaliyotibiwa kwa siku.
Mhandisi Waziri ameongeza kuwa mradi huo hautaongeza upatikanaji wa maji pekee, bali pia utafungua fursa za ufugaji wa samaki, jambo litakalochangia kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza fursa za kipato kwa wananchi wa maeneo husika.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku mkandarasi akiwa ni Kampuni ya China Jiangxi International. Ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 22 na unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Kwa wananchi wanaoathiriwa na utekelezaji wa mradi, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuwawezesha kupata makazi bora kwa kuandaa eneo jipya la makazi katika Kijiji cha Sankwaleto. Eneo hilo linaendelezwa kwa kupima viwanja na kujenga miundombinu muhimu ikiwemo shule ya msingi, nyumba za walimu, zahanati, huduma za maji, umeme na mawasiliano.
Kukamilika kwa Bwawa la Farkwa kunatarajiwa kuimarisha usalama wa maji katika Jiji la Dodoma na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.

