Habari
Mhandisi Mwajuma Awasisitiza Wataalamu Kushirikiana Katika Mradi wa Maji wa Miji 28
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka wataalamu wanaotekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Wataalamu hao ni pamoja na wasimamizi wa miradi, wakandarasi pamoja na wahandisi washauri, ambao wana jukumu la msingi katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Mhandisi Mwajuma ametoa wito huo wakati wa kikao kilichowakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Afisa kutoka Ubalozi wa India nchini Tanzania, Bw. Rajnish Kumar, pamoja na mwakilishi wa Benki ya Exim India, Bw. Ravi V. P. Singh, kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kililenga kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28, wenye thamani ya takribani shilingi trilioni 1.58, unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi milioni 6.9.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi waishio mijini na vijijini.
“Sina wasiwasi na uwezo wa wataalamu wanaotekeleza mradi huu, ila jambo la msingi ni kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa pamoja ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisema Mhandisi Mwajuma.
Ameongeza kuwa kukosekana kwa ushirikiano miongoni mwa wataalamu kunasababisha ucheleweshaji wa miradi, hali ambayo huathiri moja kwa moja maisha ya wananchi, hususan katika upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na wataalamu waliobobea katika ujenzi na usimamizi wa miradi ya maji, akisema kuwa wataalamu hao wana uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na thamani halisi ya fedha.
Mhandisi Mwajuma ameishukuru Serikali ya India kupitia Ubalozi wa India nchini Tanzania pamoja na Benki ya Exim India kwa ushirikiano wao mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 unafanikiwa.
Amesisitiza pia umuhimu wa wataalamu kutembelea maeneo ya miradi badala ya kubaki ofisini, akisema kuwa ziara za mara kwa mara husaidia kujionea maendeleo halisi ya utekelezaji wa miradi na kutambua mchango wake katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

