Habari
Ujenzi wa Bwawa la Songwe Lawakutanisha Viongozi wa Serikali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ameongoza kikao muhimu cha Makatibu Wakuu kujadili hatua za utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini pamoja na Mtambo wa Kuzalisha Nishati ya Umeme, mradi mkubwa unaolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Kikao hicho, kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Maji jijini Dodoma, kimehusisha Katibu Wakuu kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, pamoja na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe (SRBC). Lengo kuu lilikuwa kujadiliana kuhusu maandalizi ya awali ya mradi, mipango ya ushirikiano wa taasisi, na namna bora ya kuharakisha hatua za utekelezaji.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubaliana kuwa Andiko la Dhana ya Mradi (Project Concept Note) liwasilishwe mapema kwa mamlaka husika ili kuruhusu hatua zinazofuata za upembuzi yakinifu, maandalizi ya makubaliano ya utekelezaji na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi.
Bwawa la Songwe linatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi kupitia Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe. Mradi huu utachangia katika kuongeza uzalishaji wa umeme wa uhakika, kuimarisha shughuli za umwagiliaji wa kilimo, na kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa matumizi ya kaya katika wilaya za Ileje, Kyela, Momba, Mbozi na Mbeya.
Aidha, utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo husika kwa kuongeza ajira, kuimarisha shughuli za uzalishaji, na kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati na maji ya uhakika.
Mhandisi Mwajuma Waziri amesisitiza umuhimu wa uratibu wa karibu baina ya Wizara na taasisi zote zinazohusika, akibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kusimamia utekelezaji wa miradi endelevu ya maji na nishati kwa maendeleo ya taifa.