Habari
Tanzania na Polandi kuimarisha uhusiano

Tanzania na Polandi kuimarisha uhusiano
Wataalamu wa serikali kwa kushirikiana na wataalam kutoka serikali ya Jamhuri ya Polandi wamefanya kikao kazi leo kuangalia namna ya kuimarisha sekta ya maji nchini.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) aliyeongoza kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma amesema nia kuu ya kikao kazi hicho ni kuangalia maeneo ya kuimarisha ikiwamo miundombinu ya majitaka na uzalishaji wa nishati, usambazaji na menejimenti ya majisafi.
Mhe. Aweso amesema kikao kazi hicho kuhusu kuimarisha sekta ya maji kimefanyika wakati muafaka kwani wataalam wamekadiria ifikapo mwaka 2035 mahitaji ya maji nchini yataongezeka hadi kufikia mita za ujazo 57 bilioni kwa mwaka hali ambayo inahitaji kufanyia kazi na serikali mapema.
Naibu Waziri Aweso amesema hali ya huduma ya maji vijijini bado inahitaji kuimarishwa zaidi ukilinganisha na maeneo ya mijini, hivyo jitihada zaidi zinafanyika ili kuleta mabadiliko kama ilivyopangwa na serikali.
Ameongeza kuwa kikao kazi kinatarajiwa kufungua zaidi milango ya ushirikino baina ya Tanzania na Jamhuri ya Polandi, pamoja na mengine, katika maeneo matatu yanayohusu ujenzi wa miundombinu ya majitaka, uzalishaji wa nishati, usambazaji wa majisafi na mfumo wa kusimamia usambazaji wa majisafi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Polandi Mhe. Marcin Przydacz amesema nchi yao ilianza kuimarisha sekta ya maji hatua kwa hatua hadi kufanikiwa kufika katika kiwango cha hali ya juu kabisa na wako tayari kutoa uzoefu wao kwa Tanzania.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano