Habari

Imewekwa: Feb, 25 2021

Serikali yasaini Mkataba wa Bilioni 24 kupeleka maji Tinde na Shelui

News Images

Serikali kupitia Wizara ya Maji, imesaini mkataba wa kutoa maji ziwa victoria kwenda katika mji wa Tinde wilayani Shinyanga na Mji mdogo wa Shelui wilayani Ilamba mkoani Singinda, wenye thamani ya Sh. Bilioni 24.4.

Mkataba huo umesainiwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga kwa upande wa Serikali na Kampuni ya Megha Engeneering and Infrastructures LTD ya nchini India na kushuhudiwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB).

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo Waziri Aweso amewataka Wakandarasi kutekeleza mradi huo kwa wakati ndani ya muda uliopangwa wa miezi 12, na kwamba hakutakuwa na muda wa nyongeza.

“Huu ni mradi wangu wa kwanza kusainiwa nikiwa Waziri wa Maji, niwaombe Wakandarasi vipo vya kuchezea lakini siyo mradi huu, umalizeni kwa wakati na hakutakuwa na muda wa nyongeza," amesema Aweso.

Amesema licha ya kunufaisha miji midogo ya Tinde na Shelui mradi huo utanufaisha zaidi ya vijiji 30 na kwamba utekelezaji wake umetokana na agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Januari mwaka huu alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tinde akitokea Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kuzindua mradi wa maji wa Isaka-Kagongwa.

Pia amezitaka Mamlaka za Maji ambazo zitakabidhiwa kuendesha mradi huo utakapo kamilika wasitoze bili kubwa za maji, bali wafuate viwango vya bili ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti ubora wa Nishati na Maji Ewura.