Habari
Naibu Waziri Aweso Asikitishwa na Kasi ya Mradi wa Same-Mwanga

Kilimanjaro; 25 Januari, 2020
TAARIFA KWA UMMA
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesikitishwa na kasi ya wakandarasi wanaofanya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe unaotekelezwa katika Halmashauri za Wilaya za Mwanga na Same, mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri Aweso ametoa masikitiko yake alipotembelea wilaya za Mwanga na Same kukagua na kutoridhishwa na maendeleo yake, licha ya maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kwa kuwataka wakandarasi wa Kampuni za M.A Kharafi & Sons na BADR East Africa Enterprises waongeze kasi ya utekelezaji alipokagua mradi huo mwezi Julai, 2019.
“Hii ni mara yangu ya nne kufika kwenye mradi na mara ya mwisho nilikuwa hapa na Waziri Mkuu, kazi hairidhishi zaidi ya mkandarasi kutoa sababu zisizo na msingi na haiwezekani afanye kazi kwa matakwa yake’’, amesema Naibu Waziri Aweso.
“Tatizo la kukwama kwa vifaa bandarani Serikali imelitatua na makontena yote ya vifaa yameshafika eneo la kazi, mpaka sasa tumeshamlipa Dola za kimarekani milioni 71.76. Hakuna sababu yoyote ya kuendelea kutukwamisha’’, ameongeza Naibu Waziri Aweso.
Naibu Waziri Aweso ametaka kifanyike kikao haraka kati ya viongozi wa Wizara ya Maji, Halmashauri za Wilaya za Mwanga na Same pamoja wakandarasi kitakachomaliza changamoto zote na kufikia muafaka wa kumaliza kazi haraka, kitachokuwa cha mwisho na Serikali haitaendelea kuvumilia tena kasi ndogo ya mkandarasi.
Kufikia mwezi Disemba, 2019 utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 85 kwa kazi za ujenzi, asilimia 40 kwa kazi za ufundi wa mitambo na asilimia 17 kwa kazi za umeme.
Mradi wa Same-Mwanga-Korogwe ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwa takribani Shilingi bilioni 600 kwa lengo la kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa wilaya za Same, Mwanga na Korogwe pamoja na vijiji 38 vilivyopo katika eneo la mradi unaotarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 438, 931 baada ya kukamilika mwezi Machi, 2021.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini