Habari

Imewekwa: Jan, 15 2020

Mradi wa Maji Mbalika Kukamilika Mwezi Machi, 2020

News Images

Mwanza; 09 Januari, 2020

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya Ziwa Victoria kutoka tenki la maji la Mabale kwenda katika vijiji vya Nyang’homango, Isesa, Igenge na Mbalika katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.

Mradi huo unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 6 kwa fedha za Serikali ulikuwa umekwama kutokana na kuchelewa kwa upatikanaji wa mabomba na malipo ya Mkandarasi Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company, na kumlazimu Naibu Waziri Aweso kuchukua hatua ya kuidhinisha haraka fedha za ununuzi wa mabomba yote na malipo ya mkandarasi wakati wa ziara yake wilayani Misungwi mnamo mwezi Disemba, 2019.

“Nimekuja kufuatalia maelekezo niliyoyatoa nikiwa Misungwi mwezi Disemba mwaka jana, kwa ujumla kazi inaendelea vizuri na mkandarasi ameshaanza kulaza mabomba. Ninachotaka aongeze nguvukazi zaidi ili kuongeza kasi ya utekelezaji, akimsisitiza kukamilisha kazi hiyo kabla mwezi Machi, 2020’’, amesema Mhe. Aweso.

“Ni lazima mradi huu na mingine yote inayoendelea nchi nzima ikamilike haraka kwa sababu tunataka kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka huu kwa kuzindua miradi ya maji kuyafanya maadhimisho yawe na maana kwa wananchi kwa kuwafikishia huduma ya maji popote walipo’’, amesisitiza Naibu Waziri Aweso.

Aidha, mradi huo wa kimkakati utaunganishwa kutoka kwenye Kijiji cha Mbalika mpaka Kata ya Misasi ambao utahudumia zaidi ya vijiji 13 na kuwanufaisha watu zaidi ya 81,800 pindi utakapokamilika.

Naibu Waziri Aweso amekamilisha ziara ya kikazi katika mikoa ya Simiyu na Mwanza kwa kukagua miradi kwenye Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Busega, Nyamagana na Misungwi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 60.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini