Habari

Imewekwa: May, 03 2026

Wizara ya Maji Yaendesha Mafunzo Ya Uhifadhi Wa Vyanzo Vya Maji Kwa Wadau Wa Kidakio Cha Bahi

News Images

Wizara ya Maji kupitia Programu ya Uhimilivu Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Dodoma Resilient and Sustainable Water Development and Sanitation Program – DSRSWSP) inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeendesha mafunzo ya usimamizi na uhifadhi wa Kidakio cha Bahi.

Kidakio hicho ni chanzo kikuu cha Mto Bubu, unaotiririsha maji kuelekea eneo litakalojengwa Bwawa la Farkwa.

Mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Babati, mkoani Manyara, tarehe 29 Aprili 2026, yamejumuisha takriban wadau 100 wanaoishi katika eneo la juu la Kidakio cha Bahi (Upper Catchment).

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji anayesimamia Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji, Bi. Rosemary Rwebugisa, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri.

Akifungua mafunzo hayo, Bi. Rosemary amesema kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma ya majisafi nchini.

Amesisitiza kuwa, kwa upande wa Kidakio cha Bahi, uhifadhi ni muhimu ili kuhakikisha uendelevu wa Bwawa la Farkwa. “Kidakio cha Bahi ni muhimu kutunzwa ili kuhakikisha Mto Bubu unaendelea kutiririsha maji mwaka mzima kuelekea maeneo jirani na hatimaye kufika katika Bwawa la Farkwa linalojengwa Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma,” amesema.

Ameongeza kuwa tangu Serikali iutangaze Mji wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi, mahitaji ya maji yameongezeka kwa kasi. Kwa sasa, mahitaji ya maji kwa siku katika Jiji la Dodoma yanakadiriwa kufikia lita milioni 127, wakati uzalishaji wa sasa ni lita milioni 88 pekee kwa siku.

Hivyo, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi, ujenzi wa Bwawa la Farkwa ni moja ya mikakati ya muda wa kati ya kukidhi mahitaji ya maji katika Jiji la Dodoma.

Aidha, Mkurugenzi Rosemary ameielekeza Bodi ya Maji ya Bonde la Kati, ambayo ina jukumu la kusimamia Kidakio cha Bahi, kuandaa mipango jumuishi ya uhifadhi wa kidakio hicho kwa kuzingatia ushauri wa Mtaalam Mshauri. Mipango hiyo iwasilishwe Wizarani kwa ajili ya kutafuta fedha za utekelezaji.

Pamoja na mafunzo hayo, zoezi la ugawaji na upandaji miti limefanyika katika taasisi zote zinazozunguka Kidakio cha Bahi, ikiwemo shule, vituo vya afya na ofisi za umma, kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Bodi ya Maji ya Bonde la Kati.