Habari

Imewekwa: May, 03 2026

Gwandi Yaamka na Neema ya Maji! Wananchi Washusha Shukrani Kwa Serikali

News Images

Wananchi wa Kijiji cha Gwandi, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kukamilisha mradi wa maji katika kijiji hicho.

Akizungumza katika hafla fupi ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mhe. Eliasi Kawweya, amesema kukamilika kwa mradi huo ni faraja kubwa kwa wakazi wa Gwandi, kwani ni miongoni mwa miradi 18 inayotekelezwa na shirika la Water Mission katika Mkoa wa Dodoma.

Aidha, Mhe. Kawweya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa maendeleo kuendelea kutekeleza miradi ya maji wilayani humo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Mbaraka Ally, aliwapongeza wadau wa maendeleo kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo. Amesema kuwa hadi sasa, kijiji kimoja tu katika wilaya hiyo hakijafikiwa na huduma ya maji safi na salama, huku tayari kikiwa kimejumuishwa katika mpango wa bajeti ijayo.

Aidha, Mhandisi Ally alieleza kuwa mradi huo tayari umewekewa dira za malipo kabla (pre-paid meters) katika vituo vyote vya kuchotea maji pamoja na mtambo wa kunyweshea mifugo. Alibainisha kuwa mfumo huo utasaidia kudhibiti matumizi ya maji na kuondoa changamoto ya kubambikiziwa bili. Vilevile, aliwaasa wananchi kuzitunza dira hizo na kuhakikisha wanalipia huduma kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kukatika kwa maji.

Mradi huo umegharimu jumla ya Sh. milioni 577.5, ambapo kiasi cha shilingi milioni 561 zimetolewa na Shirika la Water Mission, na shilingi milioni 16.5 ni mchango wa wananchi. Mradi una mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 21.3, na unatarajiwa kuwanufaisha wananchi 5,674 wa Kijiji cha Gwandi kwa sasa, na kufikia wananchi 7,626 katika miaka ijayo.