Habari
Bodi za Maji za Mabonde Zatakiwa Kuimarisha Ufuatiliaji na Tafiti za Vyanzo Vipya vya Maji
Bodi za Maji za Mabonde nchini zimetakiwa kuimarisha ufuatiliaji wa mwenendo wa rasilimali za maji na kuendelea kufanya tafiti za kina za kubaini vyanzo vipya vya maji, hususan maji chini ya ardhi, ili kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, wakati wa kikao chake na watendaji pamoja na wataalamu wa mabonde ya maji, jijini Dodoma.
Amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimeifanya sekta ya maji kuwa katika hatari zaidi, hivyo ni muhimu kwa wataalamu hao kufuatilia kwa uhakika na kwa muda wote mienendo ya rasilimali za maji badala ya kuendelea kutegemea mito na mabwawa pekee kama vyanzo vikuu vya maji.
“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ni muhimu kufuatilia mienendo ya maji kila siku na kuacha kutegemea mito na mabwawa pekee,” Mhandisi Mwajuma amesema.
“Licha ya uwepo wa mito na mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini, bado ipo haja ya kubaini na kuendeleza vyanzo vipya vya maji vitakavyoongeza uzalishaji wa maji na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi” Mhandisi Mwajuma amesisitiza.
Mhandisi Mwajuma amefafanua kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Bodi za Maji za Mabonde ni kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali za maji, kuimarisha upatikanaji na matumizi endelevu ya maji pamoja na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia usimamizi madhubuti wa rasilimali hiyo muhimu.
Amebainisha kuwa ni wajibu wa kila mtendaji kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa rasilimali za maji.
“Naamini kupitia kikao hiki tutaweza kufanya mabadiliko chanya kwa kutumia muda wetu vyema katika kutekeleza majukumu ya utunzaji, uhifadhi na uendelezaji wa vyanzo vya maji,” ameongeza Mhandisi Mwajuma.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday, amesisitiza kuwa wataalamu wa mabonde wanapaswa kuyafahamu mabonde yao kwa undani kuanzia ngazi ya juu hadi chini, ili kuhakikisha azma na malengo ya usimamizi wa rasilimali za maji yanafikiwa kwa ufanisi na tija.

