Habari

Imewekwa: Oct, 28 2021

Wizara ya Maji yapokea Bilioni 139.4. Miradi ya maji 218 kutekelezwa

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni 139.4 kwa ajili ya Wizara ya Maji ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika kutatua changamoto ya huduma ya maji kwa Watanzania.

Video ya tukio bofya HAPA

Akizungumza na waandishi wa habari Mhe. Aweso amesema fedha hizo zimetokana na mkopo wenye masharti nafuu uliotolewa na Benki ya Dunia kupitia Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 ambapo Tanzania ilipewa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 567 sawa na takriban shilingi trilioni 1.3.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais shupavu Mhe. Samia Suluhu Hassan inatambua kwamba Maji ni rasilimali muhimu kwa ajili ya uhai wa binadamu, wanyama, mimea, mazingira na uchumi kwa ujumla. Kutokana na hilo, katika fedha hizo, Wizara ya Maji ambayo ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha Watanzania wanapata majisafi, salama na yenye kutosheleza karibu na makazi yao imepangiwa jumla ya shilingi bilioni 139.4 sawa na asilimia 10.6 ya fedha hizo.” Waziri Aweso amesema.

Ameainisha matumizi ya fedha hizo kuwa shilingi Bilioni 104 zitatekeleza jumla ya miradi ya maji 218 nchini , ambapo miradi 172 itatekelezwa mijini na miradi 46 itatekelezwa vijijini. Miradi hiyo itawezesha idadi ya wananchi milioni mbili kupata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Shilingi Bilioni 17.5 zitatumika kununua seti 25 za mitambo kwa ajili kuchimba visima ambapo kila mkoa utapata mtambo mmoja.

Shilingi Bilioni 17.6 zitatumika kununua seti tano za mitambo ya ujenzi wa mabwawa na vifaa vya utafiti wa maji chini ya ardhi ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ambayo hakuna vyanzo vya uhakika vya maji.

Amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwajali Watanzania na hasa akina mama ambao huachiwa jukumu la kuhakikisha maji yanakuepo katika makazi kwa huduma mbalimbali za kifamilia.

Waziri Aweso amewataka viongozi wa Wizara ya Maji kuhakikisha wanasimamia matumizi ya fedha hizo vizuri.

Video ya tukio bofya HAPA