Habari

Imewekwa: Sep, 16 2019

Waziri Mkuu Asisitiza Usimamizi Madhubuti wa Bonde la Mto Mara

News Images

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amezitaka mamlaka zinazosimamia Bonde la Mto Mara kwa nchi za Tanzania na Kenya kuwa na usimamizi madhubuti wa mazingira ya Bonde la Mto Mara na matumizi ya rasilimali maji katika sekta zote za kiuchumi na kijamii ili kuleta tija kwa jamii.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) alisema kuwa, wananchi zaidi ya milioni mbili wanategemea kuendesha maisha yao kupitia Bonde la Mto Mara.

Pia amezitaja changamoto zinazoikabili Sekta ya Maji hususan kwa upande wa rasilimali za maji kuwa ni uvamizi wa wafugaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, uvamizi wa wakulima kwa ajili ya shughuli za kilimo kwenye miteremko ya milima, mabonde na vyanzo vya maji, ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, mkaa na ujenzi wa nyumba mijini, umwagiliaji usiokuwa endelevu pamoja na uhaba wa kumbukumbu na takwimu sahihi kuhusiana na vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima alisema, maadhimisho ya siku ya Mara mwaka huu yamefanyika kwa ufanisi mkubwa, pamoja na kufanyika kwa warsha iliyolenga kueleza na kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi wake.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya nane (8) ya siku ya Mara mwaka huu ni “Mimi, Mto Mara-Nitunze Nikutunze” (“I, Mara River-Stand with Me”).

Kitengo cha Mawasiliano

16 Septemba, 2019