Habari

Imewekwa: Jan, 09 2021

Wahitimu wa Chuo cha Maji Kutumika katika Sekta ya Maji

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema wahitimu wa fani mbalimbali katika Chuo cha Maji inapasa watumike katika sekta ya moja ili wananchi wafaidi utaalam walioupata, hususan katika kutatua changamoto ya huduma ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Waziri Aweso amesema hayo katika mahafali ya 12 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika jijini Dar es salaam tarehe 08 Januari, 2021, ambapo alielekeza chuo hicho kipewe kazi ya ujenzi wa miradi mitano ya maji ili iwe kipimo cha wataalam wake katika kutoa huduma kwa jamii.

Mhe. Aweso aliongeza kuwa katika sekta ya maji ni lazima miradi yote inapokamilka ikabidhiwe kwa wataalam wenye weledi katika sekta ya maji na si vinginevyo, akaongeza kuwa baadhi ya miradi inashindwa kuwa endelevu kwa sababu inakabidhiwa kwa wananchi bila kuwa na wataalam wa maji wa kuwaongoza. Amesema Serikali imekamilisha jumla ya miradi ya maji 1,423 katika kipindi cha miaka mitano.

Waziri Aweso katika mahafali hayo ameambatana na uongozi wa wizara na wataalam wa sekta ya maji nchini, ambapo ameelekeza chuo kipatiwe kiasi cha shilingi milioni 750 kwa ajili ya ukarabati wa zahanati ya wanafunzi na hosteli ili wanafunzi wawe na utulivu wakati wa masomo yao.

Kufuatia agizo hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kitatolewa na Serikali ndani ya siku saba na kazi iliyokusudiwa kuanza mara moja.

Mahafali ya 12 ya Chuo cha Maji yamehusisha jumla ya wahitimu 524 wa fani tofauti tofauti zinazohusiana na sekta ya maji. Chuo cha Maji kilianzishwa mwaka 1974 na moja ya matunda yake ni viongozi mbalimbali wanaoratibu masuala mbalimbali ya sekta ya maji hapa nchini na nje ya nchi. Aidha chuo kimesaini makubaliano na RUWASA kuhusu ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini.

Wakati huohuo, Waziri Aweso ametaka mali zote za Chuo cha Maji zilichukuliwa bila kufuata utaratibu, ikiwemo ardhi na majengo, zirudishwe mara moja.

Kitengo cha Mawasiliano