Habari

Imewekwa: Feb, 22 2021

TANZANIA YAHIMIZA UTEKELEZAJI WA DIRA YA MAJI YA AFRIKA YA MWAKA 2025 (AFRICA WATER VISION 2025)

News Images

Tanzania imezihimiza nchi za Afrika kuongeza kasi ya utekelezaji wa Dira ya Maji ya Afrika ya mwaka 2025 (Africa Water Vision 2025). Hayo yamesemwa na Mheshimiwa Mhandisi Marryprisca Mahundi (Mb), Naibu Waziri wa Maji katika Mkutano wa 12 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (African Ministers’ Council on Water-AMCOW) uliofanyika tarehe 18 Februari 2021 kwa njia ya mtandao akimwakilisha Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso (Mb).

Akitoa salaam za Tanzania katika Mkutano huo uliohudhuriwa na Mawaziri mbalimbali wanaoshughulikia masuala ya maji katika nchi za Afrika, Mheshimiwa Mhandisi Marryprisca Mahundi amesema wakati umefika kwa Afrika kujizatiti na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Dira ya Maji ya Afrika ya mwaka 2025.

Dira hiyo inahusu matumizi sawia ya maji na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa ajili ya kutokomeza umasikini, kuinua maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuimarisha utangamano wa Kikanda pamoja na ulinzi wa mazingira (“An Africa where there is an equitable and sustainable use and management of water resources for poverty alleviation, socio-economic development, regional intengration, and environment”). Utekelezaji wa Dira ya Maji ya Afrika unalenga kuimarisha amani, usalama, kuondoa umaskini na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Bara la Afrika.

Akisisitiza suala hilo, Mheshimiwa Mahundi amesema kuwa utekelezaji wa Sera ya Usafi wa Mazingira ya Afrika unachangia kufikia utekelezaji wa Malengo ya Endelevu ya Umoja wa Afrika (Sustainable Development Goals-SDGs) hususani lengo Namba 6 linalohusu majisafi na usafi wa mazingira (clean water and sanitation).

Pamoja na masuala mengine, Mkutano huo umepitisha Miongozo ya Sera ya Afrika kuhusu Usafi wa Mazingira (African Sanitation Policy Guidelines). Kupitia sera hiyo, nchi za Afrika zinadhamiria kuongeza kasi ya usafi wa mazingira na uimarishaji wa afya za wananchi.

Baraza la Mawaziri wa Maji la Afrika ni Taasisi iliyo chini ya Umoja wa Afrika inayoshughulikia masuala ya maji. Baraza hilo linaundwa na Mawaziri wa Maji wa nchi zote 55 za Bara la Afrika. Lengo la Baraza hilo ni kushughulikia masuala ya Sera na Uongozi kuhusu usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji na usafi wa mazingira kwa niaba ya Umoja wa Afrika.

Aidha, linashughulikia uandaaji wa Sera, Miongozo ya Kisiasa na Mikakati ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto za upatikanaji wa maji kwa nchi za Afrika. Vilevile Mkutano huo umeshuhudia uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji ukikabidhiwa na kupokelewa na Namibia kutoa kwa nchi ya Gabon iliyomaliza kipindi chake. Tanzania imelihakikishia Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika kuwa itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu na mahiri wa AMCOW

ReplyForward