Habari

Imewekwa: Feb, 18 2021

Serikali Kupeleka Milioni 150 Kutatua Changamoto ya Maji katika Kijiji cha Izizimba A - Kwimba

News Images

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji wilayani Kwimba na kuahidi kupeleka milioni 150 kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa Izizimba A.

Ahadi hiyo ameitoa alipofika kijijini hapo kukagua mradi huo na kukuta bado haujakamilika huku wananchi wakihangaika kupata huduma ya majisafi na salama.

“Serikali italeta shilingi milioni 150 ili kazi ziendelee na nimefika hapa kutembelea miradi na kuona changamoto ili tuweze kuzitatua na kuweka msukumo ili miradi ikamilike na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza”, amesema Naibu Waziri.

Akisoma taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kwimba Mhandisi Godliver Gwambasa amesema upatikanaji wa majisafi na salama kwa Kwimba vijijini ni asilimia 56.1 na mjini ni asilimia 67.

Amesema kwa ujumla hali ya upatikanaji wa huduma ya maji unaridhisha ambapo jumla ya wakazi 269,926 kati ya wakazi 480,920 sawa na asilimia 56.1 waishio vijijini wanapata huduma ya majisafi na salama na wakazi 23,916 kati ya 35,691 wa mjini wanapata huduma ya majisafi na salama sawa na asilimia 76.

Aidha, Naibu Waziri amewataka Mameneja wa RUWASA Mikoa, Wilaya na Watendaji wote wa Wizara ya Maji kuhakikisha wanafanya kazi kwa kushirikiana ili kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji nchini.

“Mameneja wote mlioteuliwa na Mhe. Waziri wa Maji hivi karibuni hakikisheni mnakwenda kufanya kazi na kushirikiana na viongozi wa maeneo husika ili kuleta ufanisi katika kutekeleza miradi ya maji nchini”, amesema Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi.

Kwa upande wake Mbunge wa Kwimba Mhe. Mansoor Hiran ameishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya maji katika jimbo lake na kuiomba serikali kukamilisha miradi ambayo haijakamilika ili wananchi wengi wa Kwimba waweze kupata majisafi na salama.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini