Habari

Imewekwa: Jul, 10 2019

Naibu Waziri Aweso Aridhishwa na Maendeleo ya Mradi wa Maji Manispaa ya Kigoma

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wahandisi wa maji nchini kusimamia ipasavyo ujenzi wa miradi ya maji katika maeneo yao na kutowaendekeza wakandarasi wasiokidhi matakwa ya mikataba na kusababisha miradi kushindwa kukamilika kwa wakati.

Aweso ametoa maagizo hayo wakati akikagua ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kigoma katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma mara baada ya Serikali kutoa Shilingi bilioni 6 kukamilisha mradi huo baada ya kuvunja mkataba na Mkandarasi, Kampuni ya Spencon Service Ltd aliyeshindwa kukamilisha mradi kwa wakati na kuipa Kampuni ya Shanxi Construction Engineering Group Corporation Ltd.

Naibu Waziri Aweso ameridhishwa na maendeleo ya kazi hiyo na kusema kuwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa mpaka sasa imeongeza hali ya upatikanaji kufikia asilimia 69 na kuwahakikishia wakazi wa Kigoma Ujiji mpaka kufikia mwezi Oktoba, 2019 hali ya upatikanaji wa maji itafikia kiwango cha asilimia 100.

Ujenzi wa Mradi wa Maji kwenye Manispaa ya Kigoma wenye thamani ya Shilingi bilioni 33 ulianza mwaka 2013 na kutakiwa kukamilika baada ya miaka miwili, lakini umedumu zaidi ya miaka minne bila kukamilika. Hali iliyoilazimu Serikali kuchukua hatua ya kuvunja mkataba na mkandarasi wa awali na kumpa mkandarasi mwingine aweze kukamilisha kazi zilizobaki.

Aidha, Naibu Waziri Aweso ametoa miezi miwili kwa Meneja wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Mathias Mwenda kuhakikisha Mradi wa Maji wa Rukoma katika Wilaya ya Uvinza unakamilika na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Aweso ametoa agizo hilo kufuatia kusuasua kwa ujenzi wa mradi huo uliodumu kwa miaka sita badala ya miezi sita iliyoainishwa katika mkataba ilihali kiasi kikubwa cha fedha kimeshatolewa na Serikali.

Kitengo cha Mawasiliano

10 Julai, 2019