Habari

Imewekwa: Jul, 11 2019

Naibu Waziri Aweso Abaini Ubadhirifu Kwenye Mradi wa Maji Kasulu

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametoa maelekezo ya kukamatwa kwa Meneja, Kwigize Venance na Mhasibu, Joshua Hendana waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Jumuiya ya Watumia Maji ya Mradi wa Maji wa Heru Juu iliyovunjwa baada ya kubaini ubadhirifu wa fedha za mradi huo katika Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma.

Mhe. Aweso amechukua maamuzi hayo kutokana na mkanganyiko wa taarifa za viongozi wa kamati hiyo kuhusu kiasi cha fedha kilichopo kwenye akaunti ya kamati hiyo benki. Baada ya kupata maelezo ya kina akagundua mapungufu ya kamati hiyo yaliyomlazimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange kuivunja na kuamuru ufanyike utaratibu wa kupata viongozi wengine na ukaguzi wa mapato na matumizi kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Baada ya kuulizia ripoti ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya kamati hiyo kutoka kwa Mkaguzi wa Ndani, pamoja na mambo mengine ripoti imeonyesha kiasi cha Shilingi milioni 15 kimetumika kinyume na utaratibu.

"Kuna tatizo kubwa kwa upande wa usimamizi wa fedha kwenye Kamati za Watumia Maji zinazosimamia miradi ya maji vijijini, zenye jukumu la kusimamia miradi iweze kuwa endelevu. Badala ya kutumia makusanyo kwa kuendeleza miradi, yanatumika na watu wachache kwa matumizi binafsi. Nataka watu hawa wakamatwe na kurudisha fedha zote, huu uwe mfano kwa wegine", Naibu Waziri Aweso ameonya.

Wanakijiji wa Heru Juu wametoa shukrani zao kwa Naibu Waziri kwa kulipatia suluhisho tatizo hilo la muda mrefu lililosababisha wananchi kuacha kuchangia gharama za uendeshaji za mradi huo uliogharimu zaidi ya Shilingi milioni 600 kutokana na kukosa imani na kamati.

Kitengo cha Mawasiliano,

11 Julai, 2019