Habari

Imewekwa: Oct, 10 2020

Mradi wa Maji wa Chalinze-Mboga Kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi mkoani Pwani

News Images

Mradi wa Maji wa Chalinze-Mboga umelenga kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika Mkoa wa Pwanikwa kutoa huduma ya majisafi na salama kwa kuzingatia ongezeko la watu na mahitaji ya miaka 20 ijayo na kunufaisha wananchi 120,912 kwa gharama ya Sh. bilioni 14.

Mradi huu wa bomba kuu ambao ujenzi wake umefikia asilimia 78 mpaka sasa, unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo milioni tisa na laki tatu (9,300,000) kwa siku ambazo zitawezesha kuwahudumia wakazi wapatao 120,912 kwa siku.

Maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni kama ifuatavyo; maeneo ya viwanda kama vile; Viwanda vya Twyford, Kiwanda cha ngozi, Kiwanda cha Juice-SAYONA, stesheni ya treni ya mwendo kasi-Vigwaza, pamoja na maeneo yaliyoko katika mpango wa ujenzi wa viwanda .

Aidha mradi utahudumia pia maeneo ya Kijiji cha Mboga, Chamakweza, Chahua-Lukenge, Milo, Ruvu darajani, Mdaula-Ubenazomozi, Buyuni, Visezi, Vigwaza, Pingo, Pera, Bwilingu, Chalinze mjini, Chalinze Mzee na Msoga.

Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na DAWASA kwa mwaka 2019/2020 ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake za kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.