Habari

Imewekwa: Oct, 06 2021

Mradi wa Maji kigoma kuzalisha maji zaidi ya mahitaji. Utekelezaji wafikia asilimia 95

News Images

Utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma umefika asilimia 95. Mradi huo unalenga kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya laki 280 wa Manispaa ya Kigoma Ujiji pamoja na mji mdogo wa Mwandiga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) Mhandisi Mbike Jones anasema mahitaji ya wananchi wa maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka hiyo ni lita za ujazo Milioni 24 kwa siku wakati mradi huo unatarajiwa kuzalisha lita milioni 42 kwa siku. Aidha, gharama ya mradi huo inatarajiwa kufikia Euro 16,323,152.67 ambazo ni zaidi ya shilingi za Tanzania Bilioni 42 ikiwa ni ufadhili kutoka Jumuia ya Ulaya (EU).

Mhandisi Mbike amesema kwa kipindi hiki ambacho mradi huo haujakamilika Mamlaka inazalisha lita za ujazo Milioni 17 sawa na asilimia 71 ya mahitaji. Amesisitiza kuwa hatua iliyobaki ni ujenzi wa chanzo cha maji katika eneo hilo la ufukwe wa Amani, Kata ya Bangwe na shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022.

“Chanzo cha maji ya mradi huu ni ziwa Tanganyika. Nia yetu ni kuhakikisha mradi huu unakamilika ifikapo mwezi Juni 2022 hivyo wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji pamoja na Mji mdogo wa Mwandiga wasiwe na mashaka. Maji ya kutosha yanakuja muda si mrefu.” Mhandisi Mbike amesema.

Ameongeza kwa sasa asilimia 89 ya wananchi wanaohudumiwa na KUWASA wanapata huduma ya majisafi na salama. Malengo ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma hii mara baada ya kukamilika kwa mradi.