Habari

Imewekwa: Jul, 10 2019

Mkutano wa Saba wa Mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde Wafanyika Kigoma

News Images

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Waziri wa Maji Mhe.Prof.Makame Mbarawa (Mb) amefungua Mkutano wa saba wa Bodi za Maji za Mabonde unaofanyika Ujiji ,mkoani Kigoma na kuzindua taarifa ya Faida na Changamoto za Ushirikiano na Usimamizi wa Rasilimali za Maji Shirikishi pamoja naTaarifa za Rasilimali za Maji kwa ufupi (Water Resources Facts Sheet)

Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa Wizara ya Maji kufanya mikutano ya pamoja ya usimamizi wa rasilimali za maji kila mwaka kwa kuwakutanisha wataalamu wa sekta ya maji kujadiliana na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za sekta ya maji nchini na kwa mabonde ambayo ni shirikishi.

Prof.Mbarawa katika mkutano huo amewataka Wenyeviti na Maafisa Maji wa Bodi za Maji za Mabonde kusimamia kikamilifu rasilimali za maji kwa uadilifu, kudhibiti uchafuzi na kuhakikisha matumizi sahihi ya maji kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu. Pamoja na hilo amewaalika Washirika wa Maendeleo, Sekta binafsi, Taasisi na Asasi zisizo za Kiserikali kushiriki katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimaliza maji nchini kwa kuwekeza kwa kushirikiana na Wizara ya Maji.

Prof. Mbarawa amesema ili Taifa lifike katika uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda ni lazima kuwa na rasilimali za maji za uhakika.

Awali, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika mkutano huo amesema Wakala ya Usambazaji Maii na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeanza kazi ili kuleta mabadiliko na kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi vijijini. Kaulimbiu ya Mkutano huo ni “Rasilimali za Maji ni Msingi wa Maendeleo Endelevu”

Kitengo cha Mawasiliano

09 Julai, 2019