Habari

Imewekwa: Jan, 06 2021

Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Vwawa-Mlowo na Tunduma kuwa chini ya usimamizi wa RUWASA

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) ameelekeza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Vwawa-Mlowo na mji mdogo wa Tunduma mkoani Songwe kuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Songwe hadi hapo Waziri wa Maji atakapofanya uteuzi wa Wakurugenzi Watendaji wengine watakaoweza kusimamia na kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inapatikana kama ilivyokusudiwa kwa wananchi.

Amechukua uamuzi huo baada ya kukubaliana na Waziri kufuatia ziara yake aliyoifanya jana mkoani Songwe na kubaini usimamizi na uendeshaji usioridhisha wa mamlaka hizo hali ambayo imepelekea miji hiyo kuwa na changamoto ya huduma ya majisafi na salama.

Mhe. Mahundi akiwa ziarani katika Mkoa wa Songwe alikagua miradi ya maji ukiwemo mradi wa maji wa Tunduma unaohudumia kata nne za Sogea, Makambini, Mwakakati pamoja na Muungano na kubaini kuwa mradi huo unatoa maji muda mchache kwa siku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kushindwa kulipia gharama za umeme licha ya serikali kutumia Bilioni 1.3 kuutekeleza.

Aidha, katika mradi wa maji wa Vwawa-Mlowo ulio chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Vwawa-Mlowo,Serikali ilinunua pampu ya pili yenye thamani ya Shilingi milioni 100 baada ya kubaini changamoto ya pampu moja pekee iliyokuwepo ilikuwa haina uwezo kusukuma maji na kutoa huduma kwa muda wa saa 24 kwa wakazi wa miji ya Vwawa na Mlowo.

“Naibu Waziri Mahundi amesema RUWASA mkoani Songwe imeonesha kuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia na kuendesha miradi yake hivyo ni vema ikasimamia miradi hiyo wakati ikisubiri uteuzi wa Wakurugenzi Watendaji wengine.